Thursday, August 2, 2012

SOMA TAARIFA KAMILI YA AZAM KUHUSU UHAMISHO WA NGASSA


Klabu ya Azam FC inapenda kutoa taarifa ya ufafanuzi juu ya sakata la mchezaji Mrisho Ngassa ambalo linaonekana kupotoshwa

Azam FC ilitangaza kuwa biashara ya mchezaji Mrisho Ngassa ingefungwa siku ya Jumatano 1/08/2012 saa saba mchana na ilizitaka klabu zenye 'interest' na mchezaji huyo kufika makao makuu ya Azam FC, ofisi ndogo zilizopo kwenye kiwanda cha unga cha Azam-Mzizima zikiwa na pesa taslimu. Bei ya mauzo iliyopangwa ilikuwa ni dola za Marekani 50,000. Lakini katika mawasiliano ya 'email' kwa makatibu wakuu wa Simba na Yanga, Azam FC iliweka bayana kuwa ilikuwa tayari kushusha bei ya mauzo na ingemuuza Ngassa kwa timu ambayo dau lake lingekuwa kubwa zaidi ya mwenzake.

Kwa maana hiyo biashara ya mchezaji Mrisho Ngassa ilifanyika kwa uwazi. Lengo la Azam FC lilikuwa ni kutoa haki kwa kila klabu yenye uwezo wa kifedha kuweza kupata huduma ya Ngassa.

Pia tunaomba ifahamike bayana kuwa mchezaji Mrisho Ngassa alipewa taarifa kuwa anauzwa na aliombwa asaidie kushawishi klabu anayoitaka ifike kwetu na ofa yake. Ngassa alitamka bayana kuwa yupo tayari kwenda klabu yoyote ambayo Azam FC itaona imekidhi mahitaji yake kwa masharti kuwa maslahi yake ya kimkataba kati yake na Azam FC yazingatiwe.

Hadi kufikia siku ya Jumatano 01/08/2012 saa saba mchana, ni klabu ya Simba pekee iliyojibu kwa maandishi na kuonesha nia ya kumchukua Ngassa. Yanga wao hawakuwahi kujibu 'email', ingawa kwa majibu ya simu mjumbe wao wa kamati ya usajili, Seif 'Magari' alitangaza kuwa Ngassa hana thamani ya zaidi ya Sh. milioni 20. Na Yanga haikuwa tayari kuboresha ofa yake.
Muda wa kufungwa kwa biashara ya kumuuza Ngassa ulipofika, ni Simba pekee kupitia kwa makamu mwenyekiti wake Geofrey Nyange 'Kaburu' na mhasibu wake ndio waliofika wakiwa na pesa taslimu Sh. milioni 25. Yanga hawakuonekana na hawakutaka kupokea hata simu walizokuwa wakipigiwa kuulizwa kama wana 'interest'.
Kikao cha dharura cha Azam FC kilikaa na kuamua kuwa biashara ya kumuuza Ngassa ilishindikana kutokana na kutokupatikana kwa mnunuzi mwenye dola 50,000. Kwa maana hiyo Azam FC iliamua kumpeleka Ngassa kwa mkopo kwenye klabu iliyofika na kuonesha nia ya kumhitaji (Simba).
Simba walipewa sharti la kuhakikisha wanamlipa Ngassa mshahara wake kamili (Sh.milioni 2) pamoja na stahiki zake nyingine zote za kimkataba.
Sababu za kumpeleka Ngassa kwa mkopo ni kumuepusha na adhabu ambayo klabu ya Azam ingetoa kwa Ngassa kama angebaki.
Azam FC inapenda kuweka wazi kuwa haijamlazimisha Ngassa kwenda Simba kama inavyopotoshwa. Kama Ngassa anataka kuvunja mkataba wake au kama Yanga bado wanamhitaji basi waje na dola 50,000 na Azam FC itawauzia kwani licha ya kwamba amepelekwa kwa mkopo Simba lakini Ngasa bado ni mali ya Azam FC.
Tunaomba kuweka msimamo wetu kuwa hatupo tayari kumlipa Ngassa na kuvunja mkataba wake na hatuna sababu ya kufanya hivyo. Kama Ngassa hataki kwenda tunakompeleka Azam FC inamruhusu kubakia klabuni na kutumikia adhabu.
Lakini Ngasa na washauri wake waelewe kuwa akiamua kubaki Azam FC atakaa nje ya uwanja kwa muda wote uliosalia kwenye mkataba wake, kwani Azam FC haipo tayari kumvisha jezi mchezaji anayefanya vitendo vya utovu wa nidhamu.
Kwa kuwa sakata hili limeanza kuhusishwa na sakata la mchezaji Ramadhani Chombo 'Redondo', naomba nitoe ufafanuzi kama ifuatavyo. Redondo alipewa 'option' tatu za kuchagua baada ya kufanya vitendo vya utovu wa nidhamu timu ilipokuwa safarini Mwanza.
 1. Kupelekwa kwa mkopo Moro United.
 2. Kupatikana kwa mnunuzi mwenye Sh. milioni 40
 3. Kukubali adhabu ya kufungiwa kwa miezi mitatu na kulipwa nusu mshahara wahati akitumikia adhabu.

Redondo alithibitisha kuipenda Azam FC kwa kukataa kuuzwa au kupelekwa kwa mkopo. Alikubali kutumikia adhabu yake na ilipoisha alirudi na kuomba msamaha na sasa ni mmoja kati ya wachezaji wenye nidhamu ya hali ya juu sana. Azam FC inajivunia kuwa na mchezaji kama Redondo na bila kupepesa macho wala kung’ata maneno, Azam FC inamchukulia Redondo kama mtu 'spesho' na mwenye mapenzi ya dhati na klabu yake na inamtaka aendelee kuwa na moyo huo.

No comments:

Post a Comment