Friday, August 31, 2012

SIMBA WAKOMAA NA YONDANI, TWITE... YANGA YAPINGA MA-PROO WA SIMBA, AZAM YAMTAKA REDONDO WAO

Beki mpya wa Yanga, Mbuyu Twite (katikati) akiwasili jijini Dar es Salaam jana. Simba imewasilisha malalamiko ya mchezo usio wa kiungwana katika usajili wa Twite dhidi ya Yanga.

WACHEZAJI 17 wamewekewa mapingamizi ya kusajiliwa na klabu mbalimbali za Ligi Kuu msimu huu, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Simba imewasilisha malalamiko ya mchezo usio wa kiungwana katika usajili wa Mbuyu Twite aliyeko Yanga kwa maelezo alisaini mkataba na klabu yao Agosti Mosi mwaka huu mbele yao, viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Rwanda (FERWAFA) na APR ambapo alilipwa dola 30,000 na nyingine 2,000 ikiwa ni fedha ya kujikimu na nauli yake ya kujiunga na klabu hiyo.

Wekundu wa Msimbazi pia wanapinga Kelvin Yondani kusajiliwa Yanga kwa maelezo kuwa ina mkataba naye uliosainiwa Desemba 23 mwaka jana.

Yanga nayo inapinga Simba kuwaacha wachezaji Dan Mrwanda, Haruna Shamte, Kanu Mbiyavanga na Lino Masombo kwa maelezo walishapatiwa leseni za kucheza Ligi ya Tanzania walizozitumia kwenye mashindano ya Kombe la Kagame. Pia inapinga Ramadhan Chombo ‘Redondo’ kujiunga Simba kwa vile ana leseni ya kuchezea Azam kwa msimu wa 2012/2013.

Pingamizi jingine la Yanga kwa Simba ni kuwa imezidisha idadi ya wachezaji wa kigeni wanaotakiwa kusajiliwa kwa maelezo inao wanane wakati wanaoruhusiwa ni watano. Imewataja wachezaji hao kuwa ni Lino Masombo, Felix Sunzu, Emmanuel Okwi, Mussa Mude, Kanu Mbiyavanga, Pascal Ochieng, Komalmbil Keita na Daniel Akuffor.

Azam pia inapinga usajili wa Ramadhan Chombo ‘Redondo’ kwenda Simba kwa maelezo bado ina mkataba naye unaomalizika Juni 11 mwakani.

Toto Africans ya Mwanza imewawekea pingamizi wachezaji Enyinna Darlinton aliyeombewa usajili Kagera Sugar, na Mohamed Soud anayekwenda Coastal Union kwa maelezo kuwa bado ina mikataba na wachezaji hao.

Pia Flamingo ya Arusha inapinga usajili wa wachezaji wake Kelvin Friday Iddy katika timu za Azam na Salim Walii (Polisi Mara) kwa vile taratibu za kuwahamisha bado hazijafanywa. Nayo Kagera Sugar inapinga usajili wa beki David Charles Luhende kwenda Yanga kwa vile ada ya uhamisho haijalipwa.

Super Falcon ya Chanjamjawiri, Chakechake, Pemba inapinga wachezaji wake wanne; Edward Christopher Shija, Samir Said Luhava (Simba), Robert Joseph Mkhotya (African Lyon) na Sultan Juma Shija (Coastal Union) kusajiliwa katika timu hizo kwa maelezo taratibu halali za uhamisho hazikufuatwa.

Mchezaji Othman Hassan aliyeombewa usajili Coastal Union anapingwa na Oljoro JKT kwa vile bado ana mkataba na timu hiyo unaomalizika Mei 24, 2013. Nayo Rollingstone Multipurpose Ateclass Foundation ya Arusha inapinga usajili wa Kigi Makassy kutoka Yanga kwenda Simba hadi itakapolipwa fidia ya kumlea mchezaji huyo kwa vile bado hajafikisha umri wa miaka 23.

Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya TFF chini ya Mwenyekiti wake Alex Mgongolwa inatarajia kukutana kesho kupitia pingamizi hizo pamoja na usajili wa wachezaji kwa ujumla kwa 2012/2013.

No comments:

Post a Comment