Friday, August 31, 2012

YANGA KUJIULIZA KISASI CHA 5-0 KWA SIMBA OKTOBA 3

Wachezaji wa Simba wakishangilia kombe la ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu wa 2011/2012 huku wakionyesha ishara ya magoli matano baada ya kuwasambaratisha mahasimu wao Yanga 5-0 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Mei 6, 2012.
Wachezaji wa Simba wakishangilia kwa staili ya kutambaa baada ya kuwasambaratisha mahasimu wao Yanga 5-0 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Mei 6, 2012.
Wachezaji wa ikosi cha Simba kilichoifunga Yanga 5-0 wakipozi kwa picha na kocha wao Mserbia, Milovan Cirkovic, kabla ya mechi hiyo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Mei 6, 2012. Kutoka kushoto (wa pili kushoto) Mzambia Felix Sunzu, Patrick Mafisango, Haruna Moshi 'Boban', Kelvin Yondani, Uhuru Selemani, Nassoro Said 'Chollo', Mwinyi Kazimoto, Amir Maftah, Shomari Kapombe, Juma Kaseja na Mganda Emmanuel Okwi. Aliyechuchumaa ni kocha Mserbia Milovan Cirkovic. Okwi alifunga mawili, Mafisango (penalti) mbili, Kaseja (penalti) moja. Penalti tatu zilitolewa. 

Wachezaji wa kikosi cha Yanga kilichopigwa 5-0 na Simba katika mechi yao ya marudiano ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Mei 6, 2012. Waliosimama kutoka kushoto ni Oscar Joshua, Mzambia Davies Mwape, Nadir Haroub 'Cannavaro', Nurdin Bakari, Athumani Idd 'Chuji', Juma Seif 'Kijiko' na kipa Mghana Yaw Berko. Walioinama mbele kutoka kushoto ni Mganda Hamis Kiiza, Omega Seme, nahodha Shadrack Nsajigwa na Mnyarwanda Haruna Niyonzima.

Shabiki ya Yanga akibebwa na wahudumu wa msalaba mwekundu baada ya kuanguka jukwaani kufuatia kipigo cha 5-0 kutoka kwa mahasimu wao Simba kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Mei 6, 2012.

TIMU ya soka ya Yanga itapata fursa ya kwanza ya kujaribu kulipa kisasi cha kufungwa magoli 5-0 dhidi ya Simba wakati wapinzani hao wa jadi watakapokutana kwa mara ya kwanza msimu huu Oktoba 3, kwa mujibu wa ratiba ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwa msimu wa 2012/2013 iliyotolewa leo.

Simba na Yanga zilikutana kwa mara ya mwisho kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Mei 6, 2012, ambayo Yanga ilikumbana na kipigo cha 5-0 katika mechi ya mwisho ya Ligi Kuu, siku ambayo Simba tayari ilikuwa imeshatwaa ubingwa. Katika kipigo hicho cha kihistoria, Emmanuel Okwi alifunga magoli mawili, marehemu Patrick Mafisango alifunga penalti mbili na kipa Juma Kaseja alifunga penalti moja. Penalti tatu zilitolewa. 

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) leo, Ligi Kuu ya Bara itaanza Septemba 15 mwaka huu kwa timu zote 14 kujitupa kwenye viwanja tofauti.

Mechi za ufunguzi zitakuwa kati ya Simba vs African Lyon (Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam), Polisi Morogoro vs Mtibwa Sugar (Jamhuri, Morogoro), Tanzania Prisons vs Yanga (Sokoine, Mbeya), Mgambo JKT vs Coastal Union (Mkwakwani, Tanga), JKT Ruvu vs Ruvu Shooting (Azam Complex, Dar es Salaam), Kagera Sugar vs Azam (Kaitaba, Bukoba) na Toto Africans vs Oljoro JKT (Kirumba, Mwanza).

Mzunguko wa kwanza (first round) utamalizika Novemba 11 mwaka huu ambapo kwenye mzunguko huo mechi ya watani wa jadi Yanga na Simba itachezwa Oktoba 3 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ligi hiyo itamalizika Mei 18 mwakani kwa mechi kati ya Toto Africans vs Ruvu Shooting (Kirumba), Mgambo JKT vs African Lyon (Mkwakwani), JKT Ruvu vs Mtibwa Sugar (Azam Complex), Tanzania Prisons vs Kagera Sugar (Sokoine), Simba vs Yanga (Uwanja wa Taifa), Oljoro JKT vs Azam (Sheikh Amri Abeid Kaluta) na Polisi Morogoro vs Coastal Union (Jamhuri).

Endapo Simba na Azam hazitafanikiwa kuvuka hatua mojawapo ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho, ratiba hiyo itafanyiwa marekebisho.

No comments:

Post a Comment