Tuesday, August 7, 2012

RONALDO ATWAA TUZO YA MWANASOKA BORA WA DUNIA WA GOAL.COM

Cristiano Ronaldo
LOS ANGELES, Marekani
STRAIKA Cristiano Ronaldo amesema kuwa amefurahia tuzo aliyopata ya kuwa Mwanasoka Bora wa Mwaka wa Dunia inayiandaliwa na mtandao maarufu wa soka wa Goal.com, huku akiongeza kwamba anajisikia fahari kupewa heshima hiyo.

Baada ya mazoezi ya Real Madrid jana jioni jijini Los Angeles, nyota huyo wa kimataifa wa Ureno alikutana na waandaaji Goal.com na kutoa shukrani zake kwa kuchaguliwa kuwa kinara miongoni mwa wachezaji hamsini waliopigiwa kura, akiwamo hasimu wake Lionel Messi ambaye ndiye Mwanasoka Bora wa Mwaka wa Dunia wa FIFA.

“Ni suala la kujivunia kwangu baada ya kuwa mshindi wa tuzo hii," alisema mshindi huyo ambaye hii ni mara yake ya pili kutwaa tuzo hiyo ya ‘Wanasoka nyota 50 wa Goal.com’.

"Nisingeweza kupata mafanikio haya bila kusaidiwa na wachezaji wenzangu,” aliongeza Ronaldo.

Ronaldo pia alisaidia wenzake kwa kutoa pasi 15 za magoli, hivyo kuwa mmoja wa vinara wa timu yake kwa kutoa pasi za mabao.

Tangu kutua kwa kocha Jose Mourinho mwaka 2011, Cristiano Ronaldo na Real Madrid wametwaa Kombe la Mfalme na La Liga.

“Malengo yangu kwa sasa ni kucheza kwa juhudi na wenzangu ili kutwaa mataji katika kila michuano itakayokuwa mbele yetu. Sikusudii kombe moja kwa sababu nataka tupiganie kila taji, lakini ili kufanikiwa,  tunapaswa kupambana kwa nguvu zetu zote," mshambuliaji huyo aliongeza.

"Naamini kwamba kwa timu kali kama yetu, hakutakuwa na vikwazo vya kutisha mbele yetu,” alisema Ronaldo.


Cristiano Ronaldo alikuwa mhimili wa mafanikio ya Real Madrid msimu uliopita, akifunga mabao 46 katika mechi zote 38 za ligi alizocheza wakati wakiipoka Barcelona ubingwa wa La Liga, Ligi Kuu ya Hispania. Alifunga pia magoli 10 katika mechi 10 za Real iliyoishia katika hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.

TUZO YA DI STEFANO
Alikuwa mchezaji wa kwanza kuifunga kila timu ya La Liga katika msimu mmoja, huku pia akiwa mchezaji wa kwanza kufunga zaidi ya mabao 40 katika misimu miwili mfululizo ya ligi hiyo.

Kiwango chake kilitambuliwa kupitia tuzo aliyotwaa ya Trofeo Alfredo Di Stefano, ambayo hutolewa kwa mchezaji bora wa msimu wa La Liga.

Ronaldo pia alifuta dhana iliyojengeka dhidi yake kwamba hukosa makali katika mechi kubwa baada ya kuonyesha kiwango cha juu na kufunga goli la ushindi la Real Madrid dhidi ya Barcelona mwezi April na pia akang’ara katika fainali za Euro 2012.

Alifunga mara mbili na kuipa timu ya taifa ya Ureno ushindi wa 2-0 katika mechi yao ya mwisho ya hatua ya makundi dhidi ya Uholanzi, kabla hajafunga pia goli pekee lililowapa ushindi wa 1-0 katika mechi ya robo fainali ya Euro 2012 dhidi ya Jamhuri ya Czech.

Mchambuzi maarufu wa soka ambaye ni Kaimu Mhariri wa mtandao wa soka wa Goal.com, Luis Herrera, alimuelezea Ronaldo kuwa ni mchezaji ‘spesho’ aliyeipa Real ‘ubavu’ wa kuipiku Barcelona ya sasa.  

"Cristiano Ronaldo alikuwa na msimu bora zaidi baada ya kuisaidia Real Madrid kutwaa ubingwa. Kuiuzia timu ya Barcelona ya sasa unahitaji kuwa na mtu spesho na kwa mshambuliaji huyu Mreno, Real wanaye mtu huyo," alisema Herrera.
TAKWIMU ZA CRISTIANO RONALDO 2011-12


MECHI
MAGOLI
          PASI ZA MABAO
REAL MADRID
55
       60
                      15
URENO
11
       6
                      2
JUMLA
66
       66
                      17


No comments:

Post a Comment