Monday, August 6, 2012

REDONDO ARUDI SIMBA KWA DAU LA MILIONI 30/-

Redondo akishangilia bao aliloifungia Simba wakati akiichezea misimu miwili iliyopita. Je, makali yake yataonekana tena msimu ujao baada ya kurejea Msimbazi akitokea Azam leo?

Redondo akiwa kazini wakati akiichezea Azam katika mechi mojawapo za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita.
Kiungo Ramadhani Chombo 'Redondo' wa timu ya taifa, Taifa Stars amerejea katika klabu yake ya zamani ya Simba akitokea Azam kwa ada ya uhamisho inayotajwa kuwa ni Sh. milioni 30.
 

Makamu Mwenyekiti wa Simba, Godfrey Nyange 'Kaburu', amethibitisha leo kuwa ni kweli wamemsajili Redondo kwa dau hilo. 

Hata hivyo, taarifa nyingine zimedai kuwa Simba wamempatia Redondo 'advance' ya Sh. milioni 20 na kiasi kilichobaki atamaliziwa baadaye.
 
Kiungo huyo ambaye ni miongoni mwa nyota waliong'ara katika michuano iliyomalizika wiki iliyopita ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) na kuisaidia Azam kumaliza katika nafasi ya pili, amesaini leo mkataba wa miaka miwili na ataanza kuichezea tena Simba katika ligi kuu ya Bara msimu ujao.

Wakati Simba wakimsainisha mchezaji wao huyo wa zamani, taarifa nyingine kutoka ndani ya Azam zimedai kuwa klabu hiyo ya 'Wauza Koni' haijaridhia 'dili' hilo na kuna uwezekano mkubwa kuibuka mvutano mkali baina yao.

Msimu uliopita, Redondo alionyesha kiwango cha juu pia na kuisaidia Azam kupata nafasi ya kuliwakilisha taifa katika michuano ya Kombe la Shirikisho mwakani kwa mara ya kwanza baada ya kumaliza katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Bara, wakitanguliwa na mabingwa Simba.

Redondo aliwahi kung'ara vilevile wakati akiichezea Simba kabla ya kuhamia Azam misimu miwili iliyopita, katika 'dili' lililohusisha pia uhamisho wa kiungo wa kimataifa wa Rwanda aliye marehemu kwa sasa, Patrick Mafisango, ambaye alichepukia Simba akitokea Azam.       


Redondo amekwenda Simba akitokea Azam ikiwa ni siku chache tu baada ya klabu yake kumpeleka pia Ngassa kwa mabingwa hao wa Tanzania Bara kwa dau lililotajwa kuwa ni Sh. milioni 25 pamoja na gari la kutembelea alilonunuliwa straika huyo (Ngassa).

No comments:

Post a Comment