LONDON, England
MABINGWA wa Hispania, Real Madrid
walipoteza uongozi wa bao 1-0 na mwishowe kujikuta wakipata kipigo
kisichotarajiwa cha mabao 2-1 katika mechi yao ya La Liga, Ligi Kuu ya Hispania
dhidi ya majirani zao Getafe jana.
Kipigo hicho kilihitimisha kasi
yao ya kutofungwa katika mechi 24 mfululizo za La Liga na sasa wameachwa kwa
pointi tano na mahasimu wao Barcelona ambao wako kileleni mwa msimamo wa ligi
hiyo.
Gonzalo Higuain aliifungia Real
bao la utangulizi katika kipindi cha kwanza, lakini mambo yaliwabadilikia
mabingwa hao baada ya Juan Valera kufunga kwa kichwa kufutia mpira wa
"fri-kiki". Abdelaziz Barrada aliifungia Getafe goli la ushindi
wakati zikiwa zimesalia dakika 15 kabla mechi hiyo kumalizika.
Mapema juzi, Barca iliyocheza
chini ya kiwango iliokolewa na Lionel Messi aliyefunga mabao yote wakati
ikishinda 2-1 dhidi ya wachezaji 10 wa Osasuna.
Barcelona na Rayo Vallecano,
walishinda 2-1 dhidi ya Real Betis, wako kileleni mwa La Liga baada ya kila
moja kufikisha pointi sita na Real wamebakiwa na pointi moja baada ya
kushikiliwa pia kwa sare ya 1-1 katika mechi yao ya ufunguzi wa msimu dhidi ya
Valencia.
ENGLAND
Mabingwa wa Ulaya, Chelsea
waliendelea na kasi yao ya kutisha msimu huu wakati waliposhinda 2-0 Jumamosi
dhidi ya Newcastle United katika ushindi wao wa tatu mfululizo kwenye Ligi Kuu
ya England.
Chelsea, ambao wamecheza mechi
moja zaidi ya timu nyingine zote, wako kileleni mwa msimamo baada ya kufikisha
pointi tisa, tatu zaidi ya Swansea City, ambao walishinda 3-0 dhidi ya West Ham
United na Everton, ambao pia walipata ushindi wao wa pili baada ya kushinda 3-1
dhidi ya Aston Villa.
Mabingwa watetezi Man City
walipata sare ya ugenini ya 2-2 dhidi ya Liverpool, wakiokolewa na Carlos Tevez
aliyefunga bao la kusawazisha wakati akifikisha goli lake la 100 tangu aanze
kucheza kwenye Ligi Kuu ya England.
UFARANSA
Olympique Marseille wanaongoza
kwenye msimamo wa Ligue 1, Ligi Kuu ya Ufaransa baada ya kushinda 1-0 dhidi ya
mabingwa Montpellier.
Matajiri Paris St Germain walionyesha
kiwango cha chini na kuambulia sare ya nyumbani ya 0-0 dhidi ya Girondins
Bordeaux.
ITALIA
Mabingwa watetezi, Juventus
walainza vyema kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya Parma,
AC Milan wakachapwa nyumbani 1-0
katika mechi yao dhidi ya Sampdoria, Inter Milan wakishinda 3-0 dhidi ya timu
iliyopanda daraja ya Pescara huku Napoli pia wakipata ushindi kama huo mbele ya
Palermo.
UHOLANZI
Twente walishinda 3-1 dhidi ya
NEC, wakati mabingwa Ajax Amsterdam wakishinda 5-0 dhidi ya NAC Breda.
UJERUMANI
Mabingwa watetezi Borussia Dortmund na vigogo Bayern
Munich, waliendelea vyema na msimu baada ya zote kushinda katika mechi zao.
Dortmund walishinda 2-1 dhidi ya Werder Bremen huku Bayern wakishinda ugenini
3-0 dhidi ya Greuther Fuerth, waliorejea katika Bundesliga, Ligi Kuu ya
Ujerumani kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1963.
No comments:
Post a Comment