Tuesday, August 21, 2012

RAIS KAGAME, KIKWETE WAIALIKA YANGA IKULU KIGALI, DAR

Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Yusuf Manji (katikati) akizungumza wakati wa mkutano na wanahabari kwenye makao makuu ya klabu hiyo Jangwani jijini Dar es Salaam leo. Kushoto ni Makamu Mwenyekiti Clement Sanga na kulia ni Katibu Mkuu Celestine Mwesigwa.

MABINGWA wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame), Yanga wamealikwa Ikulu ya Rwanda na Rais Paul Kagame na pia Ikulu ya Tanzania na Rais Jakaya Kikwete, mwenyekiti wa klabu hiyo ya Jangwani, Yusuph Manji amesema leo.

Kutoka na mialiko hiyo, wachezaji na viongozi wa Yanga wanaondoka leo kwa ndege kuelekea Kigali kwa ajili ya kukutana na Rais Kagame na wanatarajiwa kucheza mechi tatu za kirafiki za kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Manji alisema katika mkutano wake na wanahabari, ambao ni wa kwanza tangu achaguliwe kuiongoza klabu hiyo kuwa wamefurahishwa na mialiko hiyo na kwanza wanaanza kuuitikia wa Rais Kagame na kisha utafuata wa Rais Jakaya Kikwete mara watakaporejea kutoka Kigali.

"Kama klabu tumealikwa na Rais wa Jamhuri ya Tanzania, Jakaya Kikwete, nahisi ili tupongeze (kwa kutwaa ubingwa wa klabu bingwa Afrika Mashariki na kati kwa mara ya pili mfululizo," alisema Manji.

"Sambamba na mwaliko huo, tumepokea mwaliko kutoka kwa Rais wa Rwanda Mheshimiwa Kagame wa kutembelea Rwanda na kuonana naye. Mwaliko huo umeelekeza siku na tarehe ambayo ana nafasi hiyo, ambayo ni Jumatano Agosti 22, 2012 (kesho)," aliongeza.

Manji alishasema kwamba kwamba atakuwa akikutana na wanahabari mara moja kwa mwezi.

Yanga jana ilitoa kipigo kikali cha 4-0 dhidi ya African Lyon katika mechi yao ya kirafiki kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. 

Kipa wa African Lyon, Juma Abdul akidaka wakati wa mechi yao ya kirafiki dhidi ya Yanga jana ambayo Yanga walishinda 4-0.

No comments:

Post a Comment