Tuesday, August 21, 2012

HAWA NDIO ABIRIA WA BOTI ILIYOZAMA ZANZIBAR JANA IKITOKEA TANGA... WALIELEA NA 'LIFE JACKETS' USIKU MZIMA WAKISUBIRI MSAADA, WAWILI BADO WASAKWA, FUNDI MKUU WA BOTI HIYO YA MV. SALUWAT ASIMULIA YOTE..!

Mmoja wa majeruhi akiwa kwenye Hospitali ya Kivunge jana.
Tumenusurika... raia wa Ufaransa, Benmin Luubih na Jeenle Rog wanavyoonekana baada ya kuokolewa kufuatia kuzama kwa boti waliyopanda ya Mv Saluwat.
Kweli Mwenyezi Mungu mkubwa.... mmoja wa watu walionusurika katika ajali ya kuzama kwa Mv Saluwat.
Pole sana... mmoja wa manusura wa ajali ya Mv Saluwat akiwa kwenye wodi mojawapo ya Hospitali ya Kivunge. 
Hatimaye majina ya watu wote waliokuwamo ndani ya boti ya Mv Saluwat iliyozama usiku wa kuamkia jana wakati ikitokea Pangani mkoani Tanga kuelekea Zanzibar yamefahamika  ambapo kumi kati yao waliokolewa na wengine wawili wakiendelea kusakwa.

Khalfan Saleh Ali ambaye ni mmoja wa mabaharia wa boti hiyo na abiria mmoja wa kike ambaye hadi sasa jina lake halijajulikana ndio waliokuwa wakihofiwa kufa maji kwa kuwa hadi jana jioni walikuwa bado hawajapatikana.

Waliopatikana wakiwa hai na kuwahishwa kwenye Hospitali ya Mkoa wa Kaskazini Unguja, Kivunge ni: 


1. Athumani Makame Athumani (40), mkazi wa Mtoni Kidatu-Zanzibar


2. Nahodha Ali Idi Haji (51), mkazi wa Pita na Zako-Zanzibar


3. Shaame Ali Shaame (33), mkazi wa Mtoni Kidatu - Zanzibar


4. Khamis Juma Mtwana (33), mkazi wa Kibeni - Zanzibar 


5. Ahmada Haji Kombo (47), mkazi wa Shangani Mkokotoni-Zanzibar
6. Athumani Ali Shaame (50), mkazi wa Magogoni - Zanzibar


7. Khalid Haji Maulid (49), mkazi wa Kizimbani Pita na Zako-Zanzibar.



8.  Banmin Luubih (30), raia wa Ufaransa.


9. Jeenle Rog (29), raia wa Ufaransa


10.  Ruud Verhees (23), raia wa Uholanzi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Constantine Massawe, meithibitisha kuwa boti hiyo ilizama wakati ikiitokea bandari ya Pangani juzi asubuhi kuelekea bandari ndogo ya Mkokotoni ikiwa na abiria 12 na magunia kadhaa ya nazi.

Abiria wengi ndani ya boti hiyo walinusurika baada ya wote kupatiwa makoti maalum ya uokoaji maarufu kama 'Life Jacket" na kuelea baharini kwa usiku mzima kabla ya kupatiwa msaada kuanzia jana asubuhi kutokana na jitihada za jeshi la polisi wavuvi wa bandari ndogo ya Shangani, Mkoa wa Kaskazini Ungujai.

Akisimulia safari yao ilivyokuwa hadi kuzama kwa chombo hicho, fundi mkuu wa boti hiyo ndogo, Khalid Haji Maulid, alisema iliondoka Pangani saa 2.30 asubuhi ya siku ya Jumapili. Ikaanza kupata dhoruba na kuingiza maji kuanzia saa 9:00 mchana. Fundi huyo anasema kuwa walijitahidi kuyatoa maji kwa kutumia pampu, lakini mashine hiyo nayo ilipungua nguvu kabla ya kuharibika. Fundi Khalid alisema waliamua kurudi bandarini Pangani, lakini hawakufika mbali kwani chombo hicho kinachomilikiwa na Ahmad Haji Kombo ambaye ni mkazi wa mkazi wa Shangani, Mkokotoni.
kilizidi kuingiza maji na injini yake ikazimika kabisa.

“Abiria wote tuliwapa life jackets kwa ajili ya kujiokoa. Wengine walikuwa wakielea huku wameshika chombo na waliokuwa wakijua kuogelea, walijirusha kwenye maji mapema,” alisema.

Alisema walilazimika kufanya kazi usiku kucha kuelekeza abiria wasikumbwe na mawimbi kwa kushikilia sehemu ya juu ya chombo, lakini hatimaye chombo kilizama kabisa usiku wa manane.

Fundi Khalid amesema kuwa, akishirikiana na nahodha wa boti hiyo, Ali Idi Haji, walitoa ripoti ya tukio hilo kwa vituo vya polisi wanamaji bandarini Pangani na Tanga mjini, lakini hawakupata msaada wowote haraka.

“Tuliwafahamisha tangu majira ya saa 9:00 alasiri kuwa tupo eneo la Maziwe tunahitaji msaada wa haraka, lakini bahati mbaya hadi kunakucha hatukuwaona watu wa kutupa msaada,” alisema.

Fundi Khalid alisema kutokana na kuchelewa kupata msaada wa polisi, waliwasiliana na wavuvi wanaowafahamu wanaoishi Shangani Mkokotoni.


Hata hivyo, wavuvi hao walishindwa kutoka haraka kutokana na bahari kuchafuka, hivyowalisubiri hadi usiku wa manane wakati maji yalipokupwa ndipo wakaanza safari ya kuwatafuta ili kuwapa msaada. Anasema wenzao wawili ambao hawajapatikana, walipotea alfajiri baada ya kuishiwa nguvu.

Chombo hicho kilisajiliwa na Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA) kwa namba Z907 SV kikiwa na uwezo wa kuchukua abiria 50.

Mvuvi aliyeongoza operesheni ya kuokoa watu hao, Rajabu Hamad Juma, amesema kuwa yeye alipokea taarifa majira ya saa 11:00 jioni juzi kutoka kwa watu waliokuwa kwenye boti hiyo wakiomba msaada baada ya chombo kuzidiwa na maji.

Alisema walianza safari baada ya maji kupwa usiku wa manane wakitumia tochi na taa za kandili kwenda eneo la tukio la Maziwe walikoelekezwa.


Ilipofika saa 1:00 asubuhi jana, ndipo walipowaona watu hao na walifanikiwa kuwaokoa wakiwa salama na kuwapakia katika boti yao ya Mv Tawaqal.

“Laiti kungekuwa na vyombo vya kisasa, watu hao wangeokolewa mapema zaidi,” amesema.

Kamanda wa kikosi cha Polisi wa Maji Zanzibar, Martin Lissu, amesema walipokea taarifa za tukio mapema wakiwa kituoni kwao Malindi, lakini kulikuwa na tatizo kubwa la mawasiliano kati yao na polisi wenzao wa maji wa bandari ya Tanga.

Kamanda Lissu alisema polisi wenzao wa bandari ya Tanga waliokuwa karibu zaidi na eneo la tukio walikuwa wamewaeleza kuwa wamechukua hatua za kufika eneo hilo, lakini hawakuwaona watu haraka.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa ZMA, Abdalla Hussein Kombo, amesema mamlaka yake inakabiliwa na tatizo kubwa la ukosefu wa vifaa vya mawasiliano na boti maalum za uokoaji. Akawasifu wavuvi wa Shangani Mkokotoni waliofanikiwa kutoa msaada na kuokoa abiria.

Baadhi ya walionusurika walipelekwa Hospitali ya Mkoa wa Kaskazini Unguja ya Kivunge kupatiwa huduma ya kwanza.


Tukio hili linakumbusha matukio mawili ya kuzama kwa Mv Spice Islander I Septemba 10, 2011 iliyoua takriban watu 2,000 wakati ilipozama katika eneo la Nungwi ikitokea Zanzibar kwenda Pemba na  MV Skagit iliyopinduka na baadaye kuzama Julai 18 mwaka huu katika eneo la Chumbe wakati ikisafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Zanziba na kuua watu zaidi ya 100.

No comments:

Post a Comment