Tuesday, August 21, 2012

ALICHOSEMA PETER KAFUMU BAADA YA KUVULIWA UBUNGE JIMBO LA IGUNGA LEO... CHADEMA WACHEKELEA, SASA KAZI IPO CCM....!

Peter Kafumu... sio mbunge tena wa Igunga kuanzia leo. 
Kafumu akishangilia baada ya kukabidhiwa cheti chake cha kumtambua kama Mbunge wa Igunga kufuatia uchaguzi mdogo uliofanyika jimboni humo.
Kafumu (katikati) akiinua mikono pamoja na waliokuwa wapinzani wake katika uchaguzi huo.... kushoto ni aliyekuwa mgombea wa CHADEMA, Kashindye, ambaye ndiye alifungua kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi huo na kushinda leo.
Kazi yote hii ilikuwa bure...! Kafumu akisalimiana na wananchi wakati akiomba kura kabla ya kushinda na kuwa Mbunge wa Jimbo la Tabora. Hata hivyo, kazi yote hii ilikuwa bure kwani kuanzia leo si mbunge tena wa Igunga..!  


Dalay Peter Kafumu amesema kuwa hajaridhishwa na uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Tabora wa kumvua ubunge wa Jimbo la Tabora lakini ameongeza kuwa hatachukua hatua yoyote binafsi dhidi ya hukumu hiyo na badala yake anaacha kila kitu kwa chama chake (CCM).

Akizungumza mchana huu wakati akihojiwa 'live' kwa simu kupitia kituo cha televisheni cha ITV, Kafumu alisema kuwa kamwe hakushangazwa na maamuzi yaliyotolewa leo na mahakama kuu, kwani alishajua na alishasema mara kadhaa hapo kabla kuwa jaji aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo alikuwa akiegemea zaidi upande mmoja -- ambao ni wa mlalamikaji.

Ameongeza kuwa yeye alichokuwa akikifanya wakati wote wa kampeni za kuwania ubunge ni kunadi sera za chama chake na ndio maana hajaridhishwa na uamuzi uliotolewa na mahakama leo.

"Mimi sijaridhishwa na uamuzi wa mahakama... lakini kwavile sasa si mbunge tena, nitarudi katika kazi yangu kwani mimi ni mtaalam wa madini," alisema Kafumu ambaye kabla ya kujitosa katika siasa alikuwa ni Kamishna wa Madini nchini.


Kafumu aliongeza vile vile kuwa tangu awali, alishaeleza mara kadhaa kuwa haridhishwi na jaji aliyekuwa akisikiliza shauri hilo kwa vile alikuwa akiegemea upande mmoja; na kwamba ndicho alichokifanya leo wakati akitoa hukumu.

HUKUMU LEO
Jimbo la Igunga mkoani Tabora limekuwa wazi kuanzia leo baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Tabora kumvua ubunge Dalay Peter Kafumu wa CCM kufuatia hukumu iliyotolewa katika kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi uliomuweka madarakani mbunge huyo.

Kesi hiyo ilifunguliwa na aliyekuwa mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Joseph Kashindye.

Hukumu hiyo ilivuta hisia za maelfu ya wakazi wa mji huo na maeneo ya jirani na ilianza kusomwa kuanzia mishale ya saa 3:00 asubuhi.

Pamoja na Kafumu, Kashindye pia aliwashitaki Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, Protace Mgayane . Shauri hilo lilianza kusikilizwa na Jaji Mary Nsimbo Shangali tangu Machi 26, 2012.


Awali, Hakimu Mkazi Mfawidhi Wilaya ya Nzega, Sylvester Kainda, alikaririwa akisema kuwa Mahakama Kuu kanda ya Tabora ilipanga hukumu hiyo isomwe jana lakini kutokana na siku hiyo kuwa Idd Pili, hukumu ikasomwa leo.

Profesa Abdallah Safari ambaye ni wakili wa mlalamikaji Kashindye, alisema kabla ya hukumu kutolewa leo kuwa wamewasilisha malalamiko 13 mahakamani.

Katika kesi hiyo, Kafumu alikuwa akitetewa na mawakili wawili ambao ni Antony Kanyama na Kayaga Kamaliza.

Miongoni mwa malalamiko yaliyotolewa na Kashindye katika kesi hiyo ni pamoja na vitisho katika uchaguzi huo mdogo uliofanyika baada ya kujiuzulu kwa mbunge wa zamani kupitia CCM, Rostam Aziz, mawaziri kutoa ahadi kama ya ujenzi wa daraja la Mbuntu pamoja na ahadi za kugawa mahindi kwa watu waliokuwa wakikabiliwa na njaa.

Katika hatua nyingine, mamia ya mashabiki na wanachama wa CHADEMA waliripuka kwa furaha baada ya kusikia hukumu ya kutengua ubunge wa Kafumu huku baadhi yao wakitamani uchaguzi urudiwe hata leo, wakiamini kwamba chama chao kitatwaa kiti hicho kama ilivyokuwa katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Arumeru Mashariki ambako Joshua Nassari alishinda kwa tiketi ya chama hicho.

Sasa kazi ipo kwa CCM ambayo italazimika kuketi na kuamua kama itakata rufaa kupinga maamuzi ya leo ya Mahakama Kuu Kanda ya Tabora ama la.

No comments:

Post a Comment