Monday, August 27, 2012

POLISI WAKIRI MTU MMOJA KUFA WAKATI WAKIJARIBU BILA MAFANIKIO KUZIMA MAANDAMANO YA WAFUASI WA CHADEMA MOROGORO LEO.. RPC MORO ADAI ALIYEKUFA ANA JERAHA KICHWANI, LAKINI HAWAJUI KAMA ALIPIGWA RISASI AU LA... WENGINE KIBAO WAJERUHIWA, WALAZWA...!

Hili ni moja ya bango lililotumiwa na wafuasi wa CHADEMA wakati wa maandamano ya jijini Arusha.
Viongozi wa CHADEMA walivyokuwa wakiongoza maandamano ya chama chao Arusha
Mtu mmoja aliyedaiwa kuwa ni muuza magazeti anayefahamika kwa jina la Ali Zola amefariki dunia mjini Morogoro leo wakati wa vurugu kali zilizoibuka leo kati ya wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kikosi cha kutuliza ghasia cha jeshi la polisi (FFU).

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile, amesema kuwa Zola amefariki dunia baada ya kupata jeraha kichwani ambalo hata hivyo hawajajua kuwa limetokana na kupigwa risasi ya moto ama la; lakini akidai kwamba walichofanya vijana wake (polisi) ni kuwatawanya wafuasi hao wa CHADEMA kwa mabomu ya machozi tu.

Vurugu hizo zilizokuwa gumzo mjini Morogoro leo zilitokea wakati wafuasi wa CHADEMA walipokuwa wakishinikiza kuandamana kutokea eneo la Msamvu kuelekea kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege mjini humo ambako kulikuwa na mkutano mkubwa wa hadhara.

Sakata hilo lilijiri kuanzia mishale ya saa 5:00 asubuhi ambapo maelfu ya wafuasi wa CHADEMA, huku baadhi yao wakiwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali na wengine wakiwa na magwanda ya khaki ya chama hicho, walikuwa wakisisitiza kuwa ni lazima waandamane.

Hata hivyo, FFU na polisi wa kawaida wakiwemo waliovalia kiraia walikuwa wakijaribu kuwazuia kabla ya kuanza kuwatwanga kwa mabomu kadhaa ya machozi.

Kufuatia hali hiyo, watu kadhaa walijeruhiwa na kukimbiziwa katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro ambako baadhi yao walilazwa, kabla ya kufahamika baadaye kuwa kijana  Ali Zola aliyedaiwa kuwa ni muuza magazeti maarufu amefariki dunia kufuatia kuvuja damu nyingi kichwani iliyotokana na kile kilichodaiwa na baadhi ya watu kuwa ni jeraha la risasi.

"Kafa akiwa na jeraha kichwani, hatuwezi kujua kama ni risasi au la mpaka uchunguzi ukishafanyika... ila sisi tulitumia mabomu ya machozi kutawanya waandamanaji," amesema Kamanda Shilogile.
"Tuliwaonya wananchi zaidi ya mara saba (kuwa wasiandamane)... ndipo baadaye tukatumia mabomu ya machozi kuwatawanya," ameongeza Kamanda Shilogile.

Diwani wa zamani wa Kata ya Sombetini mkoani Arusha kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Alphonce Mawazo ambaye amehamia CHADEMA, amelaani nguvu iliyotumiwa na FFU katika kuzuia maandamano hayo na kusema kuwa wao hawataacha kupambana kwa ajili mustakabali mwema wa watoto wao.

Kaimu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Hamad Yusuf, amelaani pia kile alichodai kuwa ni nguvu nyingi kupita kiasi zilizotumiwa na FFU dhidi ya wafuasi wao na kusababisha kifo na pia idadi kubwa ya majeruhi; licha ya kujua wazi kwamba kuandamana ni haki yao.

No comments:

Post a Comment