Tuesday, August 28, 2012

NIGER, GHANA ZATWAA UBINGWA AIRTEL RISING STARS

Wachezaji wa timu ya vijana ya Niger wakishangilia kombe

Nairobi, Kenya
FAINALI za michuano ya Airtel Rising Stars Afrika zimefikia tamati huku timu ya wavulana ya Niger na wasichana kutoka Ghana zikishinda ubigwa wa michuano hiyo.

Niger ilifunga Zambia 5-4 kwa mikwaju ya penati kushinda ubingwa wa kwanza wa michuano ya Airetl Rising Stars 2012 kwa wavulana. Timu hizo zilimaliza dakika 90 ya mchezo bila ya kufungana licha ya kosa kosa nyingi kwa kila timu. Hatua ya penati ilifikiwa baada ya pia kucheza dakika za nyongeza bila kufungana.

Niger walishinda penati zao zote kupitia kwa Mamane Karibou, Issa Souleymane, Abubacar Timbo, Idrissa Amadou na Issifou Garba. Timothy Sakala, Thomas Juma Mutale, Dennis Chebuye na Albert Bwalya waliifungia Zambia huku Shadrack Chimanya akikosa.

Kwa upande wa fainali za wasichana, Ghana walitoka nyuma na kuifunga wenyeji Kenya waliokuwa wakipewa nafasi kubwa ya kushinda kwa 2-1. Kenya ndio waliokuwa wa kwanza kufunga kupitia kwa Vivian Odhiambo dakika ya 27 kabla ya Emelia Lokko kushawashisha dakika ya 43. Patience Narh ndio aliepeleka kilio kwa Wakenya kwa kufunga bao la ushindi dakika ya 56.

Mechi ya fainali ilihudhuriwa na kipa wa zamani wa Manchester United, Peter Schmeichel ambaye pia amechanguliwa kuwa balozi wa klabu hiyo hivi karibu. Schmeichel ndio aliekabidhi medali kwa washindi.

Michuano hiyo ilikuwa ni moja ya mpango kambambe wa Airtel Rising Stars wenye nia ya kutafuta na kukuza vipaji vya soka kuanzia ngazi ya chini. Kwa mwaka huu, michuano hiyo ilishirikisha timu za vijana 18,000 na wachezaji 324,000 kutoka nchi 15. Pia michuano ya mwaka ilikuwa ya aina yake kwani imeweza pia kushirikisha wasichana.

Jumla ya wachezaji 432 walikuwa Nairobi kwa wiki nzima shukrani kwa kampuni ya simu za mikononi ya Airtel. Vijana hao walionyesha vipaji vya hali ya juu na ni wazi kwamba mpira wa Afrika unaelekea mahali pazuri.

Timu za Niger na Ghana zilizawadiwa fedha taslimu dola10,000 kila moja kwa kuwa bingwa. Pia timu hizo zitapata fursa kwa wachezaji wake wote kushiriki kliniki maalum chini ya waalimu wa mpira wa miguu kutoka klabu za Arsenal na Manchester United za nchini Uingereza. Kliniki hiyo itafanyika Nairobi, Kenya na Accra Ghana.

No comments:

Post a Comment