Wednesday, August 15, 2012

NI SIMBA AU MTIBWA BINGWA SUPER8

Yosso wa Simba wakishangilia KUWAKALISHA nyota wa Azam kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo.

BINGWA wa kwanza wa kihistoria katika Ligi ya Super8 anatarajiwa kuwa ni Simba au Mtibwa baada ya timu hizo mbili kutinga fainali ya michuano hiyo midogo ya kujiandaa na msimu inayofanyika kwa mara ya kwanza. 

Simba ambayo tangu mwanzo wa michuano inachezesha kikosi chao cha vijana ilishinda 2-1 dhidi ya Azam iliyojaza nyota wa timu A kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, baada ya Mtibwa kuisambaratisha Jamhuri ya Pemba kwa magoli 5-1.

Wekundu wa Msimbazi na Mtibwa watakutaka katika fainali Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, jambo linalomaanisha kwamba tayari wamejihakikishia zawadi mbili za kwanza za Sh. milioni 40 na 20.

Timu mbili zilizoishia hatua ya nusu fainali, Azam na Jamhuri, kila moja itapata Sh. milioni 15 wakati zilizobaki za Super Falcon, Zimamoto na Mtende za Zanzibar na Polisi Morogoro ya Bara, kila moja itapata Sh. milioni 5 kutoka kwa wadhamini BancABC. Benki ya ABC imesaini mkataba wa miaka mitatu na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kudhamini michuano ya BancABC Super 8 inayoshirikisha timu nane, nne kutoka Tanzania Bara na nyingine nne kutoka Zanzibar. Benki ya ABC yenye makao yake makuu nchini Botswana, na ina matawi katika nchi za Msumbiji, Zambia, Tanzania, Zimbabwe.

Jana, Simba iliandika bao lake la kwanza katika dk. 2, mfungaji akiwa Rashid Ismail kabla ya kinara wa mabao Edward Christopher kuifungia la pili na lake la tano katika mechi mechi nne kwa penalti iliyotolewa na refa Hashim Abdallah wa Dar es Salaam baada yosso huyo kuangushwa ndani ya 18 na beki wa Azam, Luckson Kakolaki.

Zahor Pazi aliyeingia katika dakika ya 66 kuchukua nafasi ya Gaudence Mwaikimba, alihitaji dakika tano tu uwanjani kuifungia Azam goli la kufutia machozi katika dakika ya 71 baada ya mabeki wa Simba kujichanganya.

Vikosi vilikuwa;
Simba:

Abuu Hashim, Miraji Adam, Omar Salum/ William Lucian (dk.80), Hassan Isihaka, Hassan Khatib, Said Ndemla, Haruna Athuman, Dullah Seseme, Edward Christopher/ Rama Mzee (dk. 84) na Frank Sekule/ Ibrahim Khatib (dk. 64).

Azam:
Jackson Wandwi, Ibrahim Chimwanga, Samir Nuhu, Said Morad, Abdulhalim Humoud, Sunday Frank/ Kevin Friday (dk. 59), Jabir Aziz/ Himid Mao (dk. 34), Abdi Kassim 'Babi', Kipre Tchetche/ Khamis Mcha (dk. 61) na Gaudence Mwaikimba/ Zahor Pazi (dk. 66).  
  

No comments:

Post a Comment