Wednesday, August 15, 2012

KAFULILA AFICHUA UFISADI WA AJABU BUNGENI JIONI HII .... ASEMA MWEKEZAJI ALIUZIWA MTAMBO WA KIWANDA NA SERIKALI KWA SH. MIL. 900; AKAACHIWA AUBEBE KWA 'ADVANCE' YA SH. MILIONI 90 TU, KISHA JAMAA AKASEPA NAO NA KWENDA KUUPIGA BEI NCHINI IRAN KWA BIL. 4.5!

Mhe. David Kafulila... haki ya nani huu ni ufisadi dhahiri. Tunataka maelezo! 
Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa... inasikitisha sana, tutachunguza.
Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, ameibua taarifa za ufisadi wa ajabu bungeni jioni hii baada ya kusema kuwa kuna mwekezaji aliuziwa Kiwanda cha Chumvi cha Uvinza kilichopo mkoani Kigoma kwa bei ya kutupa ya Sh. milioni 900 lakini bado akaishia kukitwaa kwa Sh. milioni 90 tu na kisha akang'oa mtambo mmojawapo na kwenda kuupiga bei nchini Iran kwa Sh. bilioni 4.5

Akitoa taarifa hiyo kabla ya kuuliza swali jioni hii kuelekea Wizara ya Fedha iliyokuwa ikipitishiwa vifungu vya bajeti yake jioni hii kwa mwaka ujao wa fedha, Kafulila aliitaka serikali itoe maelezo ya kutosha kuhusiana na uuzwaji wa kiwanda hicho uliojaa ufisadi.

Kafuliala akasema serikali ni lazima itoe maelezo ni kwanini imeruhusu mtambo mmojawapo ulionunuliwa kwa "advance" ya Sh. milioni 90 badala ya bei iliyotajwa ya Sh. milioni 900 ung'olewe na huyo mwekezaji na kisha kwenda kuuzwa nje ya nchi (Iran) kwa bei kubwa ya Sh. bilioni 4.5 na kuathiri shughuli za uzalishaji katika kiwanda hicho ambazo sasa zinafanywa kwa kutumia vifaa na teknolojia duni.

Aliposimama ili kujibu swali hilo, Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa, naye alionekana kushangazwa na taarifa hizo ambazo kwake zilikuwa mpya.



Dk. Mgimwa alisema kuwa taarifa hizo zinasikitisha kwani kama ni kweli, ni wazi kwamba yaliyofanyika hayaendani na masharti ya uwekezaji nchini.

"Kwanza inasikitisha. Kama mwekezaji, kwa mujibu wa masharti yaliyopo, anakwenda kufanya kitu tofauti na uwekezaji... hapo anakuwa amevunja mkataba.

"Pili, kama hayo ni kweli, kwamba mwekezaji alitakiwa kununua kwa Sh. milioni 900, akatoa advance (malipo ya awali) ya milioni 90, halafu yeye akadispose (akauza) kwa Sh. bilioni 4.5, mkataba huo unatakiwa uangaliwe... tutafanyia kazi (taarifa) ili tujue nini kilitokea," alisema Dk Mgimwa.


No comments:

Post a Comment