Thursday, August 2, 2012

NGWILIZI KUCHUNGUZA TUHUMA ZA RUSHWA DHIDI YA KINA OLE SENDEKA

*ITAWAHOJI PIA TUNDU LISSU, ZITTO KABWE

Mhe. Hassan Ngwilizi
Mhe. Tundu Lissu
Mhe. Zitto Kabwe
Mbunge wa Mlali (CCM), Mhe. Hassan Ngwilizi ameteuliwa na Spika wa Bunge kuongoza kamati ndogo ya watu watano itakayochunguza tuhuma za rushwa zinazowakabili wabunge kadhaa, wakiwamo mbunge wa Simanjiro, Mhe. Christopher Ole Sendeka na wenzake waliokuwa wakiunda kamati iliyovunjwa ya Nishati na Madini.


Uamuzi huo wa spika umetangazwa leo ili kushughulikia sakata hilo lililoibuka wakati wa mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini, ambapo ilidaiwa kuwa baadhi ya wabunge walikuwa wakitumiwa kuwatetea wafanyabiashara wa mafuta waliokosa tenda ya kuiuzia TANESCO mafuta ya kuendeshea mitambo ya kufua umeme ya IPTL.


Ole Sendeka ni miongoni mwa wabunge waliotajwa mbele ya wandishi wa habari na Mbunge wa Singida Mahsariki (CHADEMA), Mhe. Tundu Lissu kuwa naye ni miongoni mwa wanaotuhumiwa kutetea bungeni wafanyabiashara hao wa mafuta.


Hata hivyo, Sendeka aliomba mwongozo wa Spika kuhusiana na hatua hiyo ya Lissu na Spika Anna Makinda akaamuru kuwa Lissu awe shahidi namba moja mbele ya kamati ndogo atakayounda kutoka miongoni mwa wajumbe wa kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.


Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), Mhe. Zitto Kabwe, pia anatarajiwa kuhojiwa na kamati ya Ngwilizi baada ya kuwaambia waandishi wa habari jana kuwa yuko tayari kujiuzulu kuwa mwenyekiti wa kamati anayoiongoza sasa ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) pindi ikithibitika kuwa na yeye ni miongoni mwa wabunge wanaotumiwa na wafanyabiashara baada ya kupokea rushwa.







No comments:

Post a Comment