Thursday, August 2, 2012

MKOSAMALI AHOFIA KAMATI YA NGWILIZI KUWABEBA KINA OLE SENDEKA, VICKY KAMATA

Mhe. Felix Mkosamali akichangia bungeni.
Mhe. Hassan Ngwilizi
Mhe. Christopher Ole Sendeka
Mbunge wa Muhambwe (NCCR-Mageuzi), Felix Mkosamali amesema kuwa anatilia shaka uadilifu wa kamati ndogo ya wabunge watano iliyoundwa kuchunguza kashfa ya rushwa inayowakabili baadhi ya wabunge kwa vile ina wajumbe wengi wanaotoka CCM huku watuhumiwa wengi wa sakata hilo pia wakitoka katika chama hicho tawala.

Katika uteuzi wake, Spika amemteua Mbunge wa Mlali (CCM), Mhe. Hassan Ngwilizi kuongoza kamati hiyo itakayochunguza tuhuma za rushwa zinazowakabili baadhi ya wabunge, wengi  wakiwa ni wale waliokuwa katika kamati iliyovunjwa ya nishati na madini.

Mkosamali alieleza hofu yake hiyo wakati alipoomba mwongozo wa spika, na kupoendekeza kuwa kamati hiyo ya watu watano itoe mjumbe mmoja kutoka kila chama ili matokeo ya uchunguzi wake yawe ya kuaminika.

"Kati ya wajumbe watano wa kamati hii, watatu wanatoka CCM...  kwanini kila chama kisitoe mjumbe mmoja ili kamati hiyo ifanye kazi yake kwa uadilifu zaidi?" Alihoji Mkosamali.

Akitoa mwongozo juu ya  suala hilo, Mwenyekiti wa Bunge, Mhe. Jenista Mhagama, alisema kuwa spika hakukosea kuteua kamati hiyo kwani kwa mujibu wa kanuni za bunge, alitakiwa kuteua kamati hiyo ndogo kutoka miongoni mwa wabunge wa kamati inayohusika na jambo husika,  hivyo kila aliyeteuliwa miongon  mwa wajumbe hao anatoka katika Kamati ya Maadili, Haki na Madaraka ya Bunge inayoshughulikia tuhuma hizo za rushwa.

Hata hivyo, Mhe. Mhagama aliongeza kuwa kwa mujibu wa kanuni za bunge, mbunge yeyote anaruhusiwa kwenda mbele ya kamati hiyo na kuisaidia katika kutekeleza majukumu yake, bila kujali ni wa chama gani.

Spika ameunda kamati hiyo ndogo ili kubaini ukweli wa tuhuma za rushwa na pia za kutetea maslahi binafsi  zinazowakabili wabunge kadhaa waliokuwa katika kamati ya bunge iliyovunjwa ya nishati na madini.

Kati ya wanaotarajiwa kuhojiwa na kamati hiyo ni pamoja na Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA), Mhe. Tundu Lissu, ambaye juzi aliwataja mbele ya waandishi wa habari, wabunge kadhaa wa CCM kuwa ndio wanaotuhumiwa kwa rushwa, akiwamo Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka aliyedai kwamba ndiye kinara wa kuwatetea wafanyabiasha wa mafuta, Sara Msafiri, Munde Abdallah, Charles Mwijage, Mariam Kisangi na Vicky Kamata.

Kamati hiyo pia inatarajiwa kumhoji Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), Mhe. Zitto Kabwe, ambaye alisema jana kuwa yuko tayari kuchunguzwa juu ya tuhuma kwamba naye ni miongoni mwa wabunge wanaopokea rushwa na kama ikithibitika, yuko tayari kujiuzulu wadhifa alio nao sasa kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC).
.

No comments:

Post a Comment