Wednesday, August 29, 2012

MZAMBIA MAYUKA ASAJILIWA SOUTHAMPTON LEO KWA MKATABA WA MIAKA MITANO... SASA KUIVAA MAN U J'PILI

Emmanuel Mayuka... hapa akishangilia goli aliloifungia Zambia katika mechi mojawapo ya fainali zilizopita za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2012)
LONDON, England
Klabu ya Southampton inayoshiriki Ligi Kuu ya England imeongeza nguvu katika safu yake ya ushambuliaji baada ya kukamilisha usajili wa straika nyota wa timu ya taifa ya Zambia, Emmanuel Mayuka kutoka katika klabu ya Young Boys Bern ya Ligi Kuu ya Uswisi.

Straika huyo mwenye miaka 21, ambaye pia alikuwa akifukuziwa na QPR, amesaini leo mkataba wa kuichezea Southampton kwa miaka mitano baada ya jana kufuzu vipimo vya afya.   

Kocha wa Southampton, Nigel Adkins
amesema kuwa anajiandaa kumtumia Mayuka katika mechi yao ya Jumapili ya Ligi Kuu ya England watakayocheza dhidi ya Manchester United.

"Emmanuel ni straika mwenye kasi na ambaye naamini kuwa atawaletea raha mashabiki," Adkins ameiambia tovuti ya Southampton.

"Ndio kwanza ana miaka 21 lakini tayari ana uzoefu wa kutosha, hasa katika mechi za kimataifa.

"Atatuletea kitu fulani tofauti na kile ambacho tayari tunacho hapa Southampton, na tunaangalia uwezekano wa kumjumuisha kikosini kwa mara ya kwanza," amesema Adkins, kumuelezea Mayuka ambaye mabao yake yaliisaidia Zambia kutwaa ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika kwa mara ya kwanza kufuatia ushindi wao katika fainali dhidi ya timu ya taifa ya Ivory Coast iliyokuwa na nyota kibao kama Didier Drogba, Yaya Toure, Gervinho na Kolo Toure.

Mayuka ambaye ameshaichezea Zambia mara 36 tangu alipoanza kuvaa jezi za timu yake ya taifa mwaka 2007, alitwaa tuzo ya kiatu cha dhahabu katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 2012. Hadi sasa ameshaifungia Zambia mabao 10.

Mbali na Mayuka, Southampton iliyopanda daraja msimu huu na kuburuta mkia katika msimamo wa ligi baada ya kupoteza mechi zao zote mbili za mwanzo wa msimu, iko mbioni pia kumsajili winga wa Uruguay, Gaston Ramirez kutoka katika klabu ya Bologna ya Italia.

No comments:

Post a Comment