Monday, August 27, 2012

MOURINHO APONDA KIWANGO KIBOVU CHA KINA RONALDO BAADA YA REAL KUCHAPWA NA GETAFE

Huruma...! Jose Mourinho akionekana kusononeka wakati timu yake ikila kichapo katika mechi yao ya La Liga, Ligi Kuu ya Hispania dhidi ya Getafe jana. 
MADRID, Hispania
Kocha Jose Mourinho aliyekuwa amejawa na hasira ametoa kauli nadra mbele ya waandishi wa habari kuwaponda wachezaji wake wa Real Madrid baada ya kupoteza uongozi katika mechi waliyotawala muda wote na kupata kipigo kisichotarajiwa cha mabao 2-1 katika mechi yao ya La Liga, Ligi Kuu ya Hispania dhidi ya majirani zao Getafe jana Jumapili.

Kipigo hicho cha kustusha kilihitimisha rekodi yao ya miaka 15 iliyopita ya kutofungwa katika mechi 24 mfululizo za La Liga, na pia kilikuwa ni kipigo cha kwanza kwa Real katika miaka mitano kuwahi kufungwa kwenye mechi ya La Liga baada ya kuongoza hadi kufikia mapumziko.

Real walishuka dimbani baada ya sare ya nyumbani ya 1-1 katika mechi yao ya ufunguzi wa La Liga dhidi ya Valencia wiki iliyopita, hivyo sasa wameachwa kwa pointi tano na mahasimu wao Barcelona baada ya mechi mbili tu za msimu, tofauti ambayo ni kubwa baina ya klabu hizo ambazo hufukuzana hadi mwisho wa msimu.

"Real ilikuwa hovyo kabisa, ni kiwango ambacho hakikubaliki," Mourinho aliyeonekana "kufura" kwa hasira aliuambia mkutano na waandishi wa habari huku akikataa kutupia lawama mchezaji yeyote binafsi kwa kumtaja jina.

Hata hivyo, si Cristiano Ronaldo, Mesut Ozil, Karim Benzema wala Di Maria waliocheza vizuri katika siku ambayo karibu kila mchezaji wa ndani alionekana kuwa chini ya kiwango chake.

"Ujumbe pekee ninaotaka muondoke nao usiku huu ni kwamba kipigo tulichopata kilistahili," amewaambia waandishi wa habari.

"Hii ni mechi ambayo kipigo kilikuwa haki yetu kabisa. Kuambulia pointi moja katika mechi zaidi ya mbili ni balaa."

Bao la kusawazisha la Getafe lilipatikana muda mfupi baada ya mapumziko, wakati Juan Valera alipomkwepa Sergio Ramos na kuupiga mpira kwa kichwa ambao ulimpita Iker Casillas na kujaa wavuni kufuatia krosi ya 'fri-kiki'. Goli hilo linaweza kuwa moja ya sababu za kuchukia kwa Mourinho hasa kutokana na kazi kubwa ambayo ameifanya mazoezini na wachezaji wake katika kukabiliana na mipira ya adhabu.

Waliruhusu pia goli la kichwa katika mazingiora kama ya jana wakati walipokuwa wakiongoza kwa bao 1-0 dhidi ya Valencia na mwishowe kuambulia sare ya 1-1.

"Tumekuwa tukifanya kazi kubwa sana ya kujifunza namna ya kukabiliana mipira ya kutenga na sasa hakuna la zaidi tunaloweza kufanya," Mourinho amesema.

"Goli lile na jingine tuliloruhusu dhidi ya Valencia yalikuwa ni magoli  ya kipumbavu."

Mara ya mwisho kwa Real kutopata ushindi baada ya mechi mbili za La Liga ilikuwa ni msimu wa 2001-02.

Walimaliza katika nafasi ya tatu kwenye La Liga na kufungwa pia katika mechi ya fainali ya Kombe la Mfalme dhidi ya Deportivo Coruna lakini mwishowe walitwaa taji la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya baada ya kushinda katika fainali waliyocheza dhidi ya Bayer Leverkusen.

No comments:

Post a Comment