Monday, August 27, 2012

MEMBE: KUPELEKA KESI YA ZIWA NYASA MAHAKAMA YA KIMATAIFA NI GHALI SANA

Mh. Bernard Membe

WAZIRI wa Mambo ya Nje ya Ushirikiano wa Kimataifa, Mheshimiwa Bernard Membe amesema kuipeleka kesi ya kugombea Ziwa Nyasa baina ya Tanzania na Malawi ni gharama kubwa mno tofauti na watu wanavyofikiria.

Nchi ya Malawi imesisitiza jana kwamba Ziwa Nyasa lote liko katika ardhi ya nchi hiyo pamoja na sehemu ya ufukwe ulio upande wa Tanzania ni wao, kauli ambayo imepingwa vikali na Tanzania ambayo imesema mpaka wa nchi hizi mbili upo katikakati ya ziwa hiyo.

"Hatuwezi kulipeleka suala la ugomvi wa Ziwa Nyasa hivi sasa kwa sababu hiyo ni hatua ya mwisho kabisa. Kanuni za kupeleka kesi zinasema kwamba kesi itapelekwa huko ikiwa mbinu nyingine zote zimeshindikana.

"Kwanza mtazungumza baina ya pande mbili kutafuata muafaka wa suala husika, ikishindikana mnatafuta msuluhishi, yaani mtu ambaye anaaminika na pande zote mbili kwamba hatapendelea pande yoyote.

"Na katika usuluhishi wake atakachofanya msuluhishi ni kuhakikisha kwamba kila upande unaridhika na upatanisho wake si kuupa upande mmoja ushindi. 

"Kupeleka kesi katika mahakama ya kimataifa si jambo dogo. Linahitaji kila upande kukusanya vielelezo vyote vikiwamo vya kihistoria kutoka kwa mababu na viongozi wa zamani kuona namna walivyokuwa wanalichukulia ziwa hilo. Isije ikawa mabadiliko yalifanywa na mlevi mmoja tu. Maana anaweza akaibuka mlevi mmoja tu akaamua kusema tofauti na ambavyo imekuwa ikichukuliwa kwa miaka yote tangu enzi za mababu.

"Halafu kesi katika mahakama ya kimataifa inachukua muda usiopungua miaka miwili hadi kumalizika. Na kwa siku kuiendesha inagharimu kati ya dola 10,000-12,000 (Sh. milioni 15.5 hadi Sh. milioni 18.5 kwa siku)," alisema Membe.

Alisema kutokana na mambo hayo wanachoangalia kwa sasa ni kufuata taratibu za awali za mazungumzo baina ya pande mbili ili kulipatia ufumbuzi suala hilo.

Membe alisema hayo wakati akihojiwa na kipindi cha "Power Breakfast" cha kituo cha Radio cha Clouds FM asubuhi ya leo.


No comments:

Post a Comment