Monday, August 20, 2012

MBWANA SAMATTA AACHA GUMZO KUBWA MISRI... NI BAADA YA KUZIPIGA MABAO ATAKAVYO KLABU ZAO VIGOGO ZA ZAMALEK NA AL AHLY.... SASA ABAKIZA GOLI MOJA TU KUWASHIKA ABOUTRIKA NA TRESOR MPUTU.....!

Samatta akipiga mahesabu ya kumtoka beki wa Zamalek

Goooooooooooohhh.....! Chezea Samatta wewe.... hapa 'dogo' anafunga bao la pili lililoing'oa Zamalek katika michuano ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika jana.

Huyu dogo noma sana. Sijui kaja ni vizizi vyake kutoka kwao Mbagala? Kipa wa Zamalek akiwa hoi baada ya kupigwa bao 'kali' na Samatta.

Aiya weee.... basi tena! Kipa wa Mazembe akijutia baada ya kushindwa kuokoa mpira wa kichwa cha Samatta jana
CAIRO, Misri
STRAIKA wa kimataifa wa Tanzania amezua gumzo kubwa nchini Misri baada ya jana kuendeleza rekodi yake ya kuzipiga mabao klabu vigogo za nchi hiyo wakati alipofunga goli kali la kichwa na kuipa timu yake ya TP Mazembe ushindi wa 2-1 dhidi ya Zamalek kwenye uwanja usio na mashabiki jijini Cairo nchini humo.

Chanzo cha gumzo la Samatta miongoni mwa mashabiki wa soka nchini Misri ni uwezo wake mkubwa wa kumiliki mpira, kuwatoka mabeki na kutumia vyema nafasi anazopata katika kufunga, hasa katika mechi tatu zilizopita za ligi ya klabu bingwa Afrika ambapo klabu yake ilicheza dhidi ya klabu vigogo nchini humo za Al Ahly na Zamalek.

Kabla ya mechi ya jana, Samatta aliwasumbua sana mabeki wa Al Ahly na kufunga kwa kichwa bao pekee la Mazembe wakati klabu yake ikilala 2-1 katika mechi ya kundi lao la B iliyochezwa nchini Misri. Wiki mbili zilizopita, Samatta aliwapelekesha kadri alivyotaka mabeki wa Zamalek ambao ni mahasimu wa jadi wa Ahly na kufunga bao mojawapo kali la kichwa wakati wakishinda nyumbani 2-0.

Na jana tena, Samatta alikuwa ni mmoja wa nyota wa Mazembe waliowanyima raha mabeki wa Zamalek na kuwakosakosa zaidi ya mara mbili kabla ya kupiga goli 'tamu' la kichwa liliwapa ushindi wa 2-1 na kuing'oa Zamalek katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika.

Rekodi hiyo ya muda mfupi, akipiga magoli matatu kwa kichwa katika mechi tatu zilizopita dhidi ya klabu vigogo za Misri, ndio chanzo cha mjadala wa Samatta nchini Misri.

Katika mechi ya jana usiku iliyochezwa kwenye uwanja usio na mashabiki kwa sababu za kiusalama, nahodha wa Mazembe, Tresor Mputu ndiye 'aliyetengeneza' mabao yote ya Mazembe.

Kona ya Mputu katika dakika ya 34 iliunganishwa vyema kwa kichwa kilichopigwa na Mzambia Hichani Himoonde na kuwapa wageni bao la utangulizi. Dakika moja baadaye, Zamalek wakasawazisha kupitia kwa nyota wa kimataifa wa Benin, Razak Omotoyossi, ambaye aliudokolea wavuni mpira wa krosi ya chini kutoka wingi ya kushoto uliotoka kumpita kipa veterani, Robert Kidiaba.

Samatta aliifungia Mazembe bao la ushindi kwa kuunganisha vyema krosi nzuri ya Mputu wakati zikiwa zimebaki dakika chache kabla ya mapumziko.

Bao hilo la jana, sasa limemfanya Samatta afikishe jumla ya mabao matano katika michuano hiyo na kuendelea na kasi nzuri ya kufukuzia kiatu cha dhahabu, akibakiza goli moja tu kuwashika nyota Tresor Mputu wa klabu yake ya Mazembe na Mohamed Aboutrika wa Ahly ambao kila mmoja amefikisha mabao sita huku megine yakitokana na penati. Mghana Emmanuel Clottey wa Berekum Chelsea ya Ghana yuko kileleni mwa orodha ya wafungaji baada ya kufunga mabao 12 huku matatu yakitokana na penati.

Kufuatia ushindi wa jana, Mazembe wamefikisha pointi saba na kukamata nafasi ya pili kwenye msimamo, pointi tatu nyuma ya Al Ahly wanaoongoza kundi lao la B. Chelsea ya Ghana inaifuatia Mazembe baada ya kufikisha pointi tano na Zamalek inaburuza mkia kwa kutokuwa na pointi huku kila timu ikiwa imebakiza mechi mbili kumaliza mechi za hatua ya makundi.

Ahly ilishikiliwa na Chelsea kwa sare ya 1-1 mjini Accra jana na baada ya kuwahi kuongoza kwa tofauti ya pointi tano wiki mbili zilizopita, sasa hawana tena uhakika wa kumaliza kileleni mwa kundi hilo, ingawa tayari wameshajihakikishia nafasi ya pili na kutinga nusu fainali.


Vinara wa ufungaji Klabu Bingwa Afrika:
                                                                       Magoli      Penati
Emmanuel Clottey    (Berekum Chelsea)        12              3
Mohamed Aboutrika  (Al Ahly)                        6               2  
Tresor Mputu            (TP Mazembe)                6               1
Mbwana Samata       (TP Mazembe)                 5               0
Isu Azuka                 (Sunshine)                        5               0
      

No comments:

Post a Comment