Monday, August 20, 2012

ALEX SONG ATUA MJENGONI BARCELONA... WENGER ASEMA INAUMA LAKINI SIO ISHU SANA KWAVILE ARSENAL INA VIUNGO KIBAO KAMA DIABY, WILSHERE, ROSICKY…!


Yaap, hapa nilipotua nd'o penyewe... ntapata umateumate wa ukweli na makombe ntabeba mpaka makwapa yaniume! Kiungo Alex Song akipozi kwa picha leo ndani ya mjengo wa Barcelona nchini Hispania.  
Alex Song akiwa kwenye mjengo wa klabu ya Barca leo asubuhi.

Mzukaaaaa....! Mbwembwe za Alex Song baada ya kutua kwenye mjengo wa Barca leo.
BARCELONA, Hispania
Kiungo aliyekuwa Arsenal, Alex Song anatarajiwa kusaini mkataba wake wa kuichezea Barcelona kwa miaka mitano baada ya kutambulishwa rasmi leo katika tukio la kuchukuliwa kwa vipimo vya afya.


Kiungo huyo wa kimataifa wa Cameroon mwenye miaka 24, yuko mbio kusaini mkataba huo baada ya klabu yake ya Arsenal kukubali ‘dili’ la kumuuza kwa paundi za England milioni 15 (Sh. bilioni 37)

Taarifa iliyotolewa leo na Barca imeeleza kuwa baada ya kusaini mkataba wake, kiungo huyo atatambulishwa mbele ya waandishi wa habari kesho.

Song hakucheza juzi Jumamosi katika mechi ya Arsenal ya ufunguzi wa Ligi Kuu ya England dhidi ya Sunderland iliyomalizika kwa sare ya 0-0, na baadaye Arsenal kuthibitisha kuwa wamekubali kumuuza kiungo huyo kwa Barca.

"Siku zote huwa inauma kupoteza wachezaji wazuri, lakini tuna wachezaji wengi katika eneo la kiungo," alisema kocha wa Arsenal, Arsene Wenger.

"Tunaangalia pia uwezekano wa kuleta kiungo mwingine mmoja, na pengine beki mwingine mmoja pia kwa sababu tunadhani kwamba bado tuna upungufu katika baadhi ya maeneo," alisema Wenger, huku taarifa zikidai kwamba wanamfukuzia kiungo asiye na nafasi katika klabu ya Real Madrid, Nuri Sahin.

Miongoni mwa viungo kibao ambao Wenger anajivunia ndani ya kikosi chake cha Arsenal ni pamoja na Abou Diaby, Jack Wilshere, Tomas Rosicky na Santi Cazorla aliyemsajili msimu huu akitokea Malaga.

Song, aliyekuwa amebakiza miaka miwili kumaliza mkataba wake, alijiunga na Arsenal wakati akiwa na miaka 17 akitokea katika klabu ya Bastia ya Ufaransa mwaka 2005.

Awali alitua kwa mkopo wa mwaka mmoja, kisha akapewa mkataba wa kudumu baada ya kutwaliwa jumla kwa ada ya paundi za England milioni 2.75 (Sh. bilioni 7)

Hivi karibuni, Arsenal pia waliwasajili mastraika Olivier Giroud na Lukas Podolski, lakini vilevile wakimpoteza nahodha wao Robin van Persie waliyemuuza kwa Manchester United kwa ada ya paundi za England milioni 24 (Sh. bilioni 60).

No comments:

Post a Comment