Thursday, August 2, 2012

MBUNGE BARWANI AHOJI KAMA DK. MWAKYEMBE ANAKOMALIA BANDARI BAGAMOYO ILI KULIPA FADHILA ZA KUPEWA UWAZIRI

Mhe. Salum Barwani
Mhe. Dk. Harrison
Mbunge wa Jimbo la Lindi Mjini (CUF), Mhe. Salum Barwani, ameishangaa Wizara ya Uchukuzi inayoongozwa na Dk. Harrison Mwakyembe kwa kusema kuwa itajenga bandari mpya ya Bagamoyo wakati zile zilizopo kama ya Lindi zikitelekezwa.

Mhe. Barwani ameyasema hayo bungeni leo wakati akichangia hoja ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka uijao wa fedha, ambapo alienda mbali zaidi na kuhoji kama mpango huo unatokana na nia ya Waziri na wenzake kulipa fadhila kwa watu waliowapa madaraka waliyo nayo.

"Mnasema mnataka kujenga bandari mpya ya Bagamoyo, hizi zilizopo mmeshaziboresha? Au mnataka kulipa fadhila kwa watu waliowaweka kwenye madaraka?" Alihoji Mhe. Barwani bila kufafanua zaidi na kuzua shangwe kwa wabunge wenzake wa upinzani, pengine kutokana na ukweli kwamba mteuzi wa Dk. Mwakyembe kwa nafasi aliyo nayo ni Rais Kikwete ambaye kwao ni Bagamoyo.

Wakati akichangia mjadala huo, Mhe. Barwani pia aliitaka serikali ieleze ni kwanini inaonekana kuitenga mikoa ya Lindi na Mtwara katika uboreshaji wa miundombinu (kama bandari ya Lindi), huku akionya kuwa hali hiyo si nzuri kwani inaweza kuibua hisia mbaya kwa watu wa maeneo hayo dhidi ya serikali na mwishowe kuhatarisha hali ya umoja na mshikamano wa taifa.

No comments:

Post a Comment