Sunday, August 12, 2012

MAN CITY YAIPIGA CHELSEA, YABEBA NGAO YA JAMII

Beki wa Manchester City, Alexandar Kolarov akibeba Ngao ya Jamii baada ya kuifunga Chelsea kwenye Uwanja wa Villa Park mjini Birmingham leo. Picha: REUTERS

Nahodha Vincent Kompany akiinua juu Ngao ya Jamii waliyoitwaa baada ya kuifunga Chelsea 3-2. Picha: REUTERS

Wachezaji wa Man City wakishangilia baada ya kuifunga Chelsea 3-2. Picha: REUTERS
Carlos Tevez akifungua shampeni baada ya kubeba Ngao ya Jamii. Picha: REUTERS
Nigel de Jong akigonga shampeni kwa mtindo wa tarumbeta... wapi mhudumu ampelekee glasi? Picha: REUTERS
Hoii... chezea Man City wewe? John Terry akijiuliza baada ya kipigo. Picha: REUTERS

Beki Branislav Ivanovic (kulia) akilimwa kadi nyekundu baada ya kumchezea rafu mbaya Kolarov aliyekaa chini. Picha: REUTERS

Tumebeba ubingwa msimu uliopita na sasa tumeanza na Ngao ya Jamii, mtatukoma mwaka huu..... Wachezaji wa Man City wakishangilia baada ya kuifunga Chelsea 3-2. Picha: REUTERS

Frank Lampard (kulia) wa Chelsea akijaribu kuosha mpira mbele ya Samir Nasri wa Manchester City wakati wa mechi yao ya Ngao ya Jamii kwenye Uwanja wa Villa Park mjini Barmingam leo. Man City ilishinda 3-2. Picha: REUTERS

LONDON, Uingereza
MANCHESTER City inaweza kuwa haijasajili nyota wapya wenye majina makubwa msimu huu, lakini walituma ujumbe kwa mahasimu wao wa Ligi Kuu ya England kufuatia ya ushindi wa 3-2 dhidi ya Chelsea iliyobaki na wachezaji 10 katika mechi yao ya Ngao ya Jamii leo jioni.

Kutokana na Uwanja wa Wembley kuwa 'bize' kwa Michezo ya Olimpiki, Uwanja wa Villa Park wa Birmingham ndio uliotumika kwa mechi hiyo ya kitamaduni ya ufunguzi msimu wa England, ambayo iliwakutanisha mabingwa wa ligi Man City dhidi ya mabingwa wa Kombe la FA na Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya Chelsea, wiki moja kabla ya kuanza kwa msimu wa Ligi Kuu.

Chelsea imetumia zaidi ya paundi milioni 60 katika kipindi cha sasa cha usajili wakati Man City mchezaji pekee iliyemnunua ni Jack Rodwell wa Everton, tena dili ambalo limekuja kufahamika saa chache kabla ya kuanza kwa mechi hiyo.

Hata hivyo magoli kutoka kwa Yaya Toure, Carlos Tevez na Samir Nasri ndani ya kipindi cha dakika 12 za kipindi cha pili yalidhihirisha kwamba timu hiyo tayari ni "muziki mnene".
Walisaidiwa na kutolewa kwa kadi nyekundu kwa beki wa Chelsea, Branislav Ivanovic katika kipindi cha kwanza kutokana na rafu aliyocheza dhidi ya Aleksandar Kolarov.

Man City, iliyotumia mfumo wa 3-4-3, ilianza vyema lakini tofati na mwelekeo wa mchezo Chelsea walipata goli la kuongoza dakika tano kabla ya mapumziko wakati Fernando Torres alipofunga kwa shuti la nje ya kiatu chake cha kushoto baada ya pasi "tamu" ya Ramires.

Haikuwachukua muda mrefu Man City kutumia mapungufu ya wachezaji uwanjani baada ya kadi nyekundu ya Ivanovic pale Yaya Toure, Tevez na Nasri walipoipa timu yao uongozi mzuri wa magoli 3-1 yaliyofungwa kiufundi.

Ryan Bertrand, aliyechukua nafasi ya mchezaji mpya Eden Hazard, aliwafungia goli jingine moja mabingwa wa Ulaya katika dakika ya 80, akicharuka haraka zaidi wakati kipa wa Man City, Costel Pantilimon alipoutema kizembe mpira uliopigwa na Daniel Sturridge, lakini tayari vijana hao wa Roberto di Matteo walikuwa wamekumbuka shuka wakati kumeshakucha.

------------

No comments:

Post a Comment