Wednesday, August 8, 2012

LUCAS MOURA AKIRI KWENDA PSG AKIITOSA MAN UTD

Lucas Moura

Lucas Moura wa Brazil akifanya vitu vyake katika mechi mojawapo ya michezo ya Olimpiki inayoendelea jijini London. 
SAO PAULO, Brazil
LUCAS Moura amekiri kwamba anaweza kuihama klabu yake ya Sao Paulo na kujiunga na Paris Saint-Germain inayoshiriki Ligue 1, Ligi Kuu ya Ufaransa katika kipindi cha usajili wa dirisha dogo la Januari.

Kiungo-mshambuliaji huyo ameendelea kuhusishwa na uhamisho wa kwenda Ulaya, huku klabu za Manchester United na Inter zikimfuatilia kwa karibu ili kumnyakua yosso huyo mwenye miaka 19 kutoka katika klabu yake ya sasa.

Hata hivyo, Man U na Inter haziko tayari kulipa dau kubwa linalotakiwa na Sao Paulo kwa ajili ya Lucas, hivyo kuipa nafasi PSG kuwa katika nafasi nzuri ya kushinda mbio za kuwania saini ya nyota huyo wa kimataifa wa Brazil.

"Nimezungumza na Thiago Silva na Leonardo, wamenisimulia mambo mengi mazuri kuhusiana na klabu hiyo na mipango wanayoitekeleza. Mazungumzo yanakwenda vizuri, lakini bado hayajakamilika," Lucas ameiambia Globo Esporte.

"Nitabaki Sao Paulo hadi mwisho wa msimu. Mara zote nimekuwa nikisema kwamba ninataka kutwaa ubingwa na kufuzu kwa michuano ya Copa Libertadores (Ligi ya Klabu Bingwa Amerika Kusini) kabla ya kuondoka.

"Kama uhamisho utatokea Januari, nitakuwa tayari kufanya hivyo kwa ajili ya Sao Paulo. Hata hivyo, kwa sasa, naangalia zaidi timu ya taifa. Naweza tu kuzungumzia jambo hili baada ya  Olimpiki."

PSG hivi sasa imeshatimiza idadi inayoruhusiwa ya wachezaji wanne wasiokuwa raia wa Ulaya katika kikosi chake, lakini ina matumaini kwamba Milan Bisevac atapata uraia wa nchi mbili katika muda mfupi ujao, hivyo kuipa nafasi ya kuongeza mchezaji mwingine mmoja wa nje ya Umoja wa Ulaya katika kikosi chake katika kipindi cha sasa cha uhamisho wa majira ya kiangazi au Januari.

No comments:

Post a Comment