Wednesday, August 8, 2012

BARCELONA WAFIKIA MAKUBALIANO NA ALEX SONG KUHUSU MSHAHARA NA MASLAHI MENGINE BINAFSI

Alex Song, kiungo nyota wa Arsenal anayetarajiwa kuvaa 'uzi' wa Barca katika msimu ujao wa La Liga, Ligi Kuu ya Hispania
LONDON, England
DHAMIRA ya klabu ya Barcelona kumnasa kiungo Alex Song wa Arsenal inaelekea kutimia baada ya vigogo hao wa Hispania kufikia mwafaka wa malipo binafsi ya kiungo huyo wa kimataifa wa Cameroon ikiwa ni pamoja na mshahara watakaomlipa kwa wiki, imefahamika leo.

Gazeti la Michezo la Sport limesema kuwa Barca pia wameshafikia makubaliano na Song kuhusiana na mkataba wake na sasa wameanza harakati za kumalizana na Arsenal ili wawalipe chao wiki hii na kumtwaa jumla kiungo huyo aliyeng'ara msimu uliopita.

Imeelezwa zaidi kuwa maafikiano ya haraka yanatarajiwa kupatikana, ingawa inaaminika vilevile kuwa 'dili' hilo linaweza kukamilika wiki ijayo.

Arsenal wamekuwa wakiitaja bei ya Song sokoni kwa sasa kuwa ni paundi za England milioni 16. Kiwango hicho hakitarajiwi kuitisha Barca ambayo imepania kumtwaa Song ili azibe nafasi iliyoachwa wazi na kiungo wa kimataifa wa Mali, Seydou Keita, ambaye amehamia katika ligi kuu ya China hivi karibuni na kuwaacha mabingwa hao wa zamani wa Ulaya wakibaki na kiungo mkabaji wa uhakika mmoja tu -- Sergio Busquet.

 Mchezaji mwingine wa nafasi ya Busquet katika kikosi cha Barca, Muargentina Javier Mascherano, amekuwa akitumika kama beki wa kati na kuonyesha kiwango cha juu. 

No comments:

Post a Comment