Friday, August 3, 2012

JUVE WACHOSHWA NA ‘SITAKI NATAKA’ ZA VAN PERSIE, WATAKA KUFIKIA JUMANNE AWAPE JIBU ‘YES’, AU ‘NO!’


Van Pesrie akishangilia baada ya kuifungia Arsenal goli katika mechi mojawapo ya Ligi Kuu ya England dhidi ya Wigan msimu uliopita.   
TURIN, Italia
Klabu ya Juventus ya Italia imemtaka straika wa Arsenal, Robin van Persie aache ‘longolongo’ na kumtaka awape haraka jibu la kueleweka kuwa ataihama klabu yake ya sasa na kujiunga nao ama la!

Gazeti la The Mirror limesema kwamba Juventus wameshachoshwa na hali ya kuwekwa njia panda na hivyo wamemwambia Van Persie kupitia wakala wake Kees Vos kuwa wanamtaka hadi kufikia Jumanne ijayo (Agosti 7) awe tayari ameshatoa jibu la kueleweka kuhisiana na hatma yake -- na kwamba vinginevyo, wao watajitoa katika mbio za kumuwania na kutafuta straika mwingine badala yake.

Mabingwa hao wa Serie A, Ligi Kuu ya Italia, wamesema kuwa wamechoka kumsubiri Van Persie, hasa baada ya kusikia kuwa swahiba wa Vos, Carl Thomas, ameandika kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba, kwavile kocha wa Juve, Antonio Conte anakabiliwa na adhabu ya kufungiwa kwa muda mrefu kutokana na kashfa ya upangaji matokeo, sasa “itakuwa ngumu” kwa straika huyo kucheza katika Serie A.

Ofa ya kwanza ya Juventus ya kumtwaa Van Persie ilikataliwa na inaeleweka kwamba wameshatuma ombi jingine lililokataliwa pia, ingawa wameeleza wazi kuwa wako tayari kumpa straika huyo mkataba wa miaka mitano utakaomhakikishia mshahara mnono wa paundi za England 190,000 (Sh. milioni 460) kwa wiki.

No comments:

Post a Comment