Saturday, August 11, 2012

JOE ALLEN AKAMILISHA USAJILI LIVERPOOL

Joe Allen

LIVERPOOL imekamilisha usajili wa kiungo wa kimataifa wa Wales, Joe Allen, kutoka klabu ya Swansea City.

Allen, 22, alikuwamo uwanjani Anfield Alhamisi wakati Liverpool ikiifunga FC Gomel 3-0 na akafuzu vipimo vya afya jana Ijumaa.

Amekuwa mchezaji wa pili kusajili chini ya kocha mpya Brendan Rodgers baada ya kutua kwa mshambuliaji wa kimataifa wa Italia, Fabio Borini, kutoka AS Roma.

"Najisikia furaha sana. Kila mmoja anafahamu historia yaklabu hii, ni klabu kubwa sana, na nina furaha kujiunga nayo," aliiambia tovuti ya klabu hiyo.

"Mzuka walionao watu hapa katika soka ni jambo ambali liko kwangu pia na nataka kuwa sehemu ya hilo.

"Najiandaa kuwa sehemu ya miaka ya kukumbukwa ijayo Liverpool."

Rodgers anaamini Allen atakuwa injini kwa kuingiza staili yake ya kucheza katika timu ya Liverpool.

Allen alikuwa muhimu katika mfumo wa uchezaji wa Rodgers wakati wakiwa pamoja Swansea na anatarajia kiungo huyo atafanya hivyo pia Anfield.

"Nina furaha sana kwamba Joe ameamua kuja kujumuika nasi katika safari hii," Rodgers alisema.

"Joe ni mchezaji ambaye uwezo wake unaendana na mawazo ya kikundi hiki. Uwezo wake kumiliki na kutawala mpira ni jambo muhimu katika majaribio yetu ya kupata mafanikio uwanjani.

"Joe alipata somo zuri alipokuwa Swansea City na sasa ataanza ukurasa mpya katika maisha yake mazuri ya soka."

Klabu hizo mbili zilianza mazungumzo juu ya Allen mwezi uliopita, lakini ofa ya awali ya klabu hiyo ya Anfield ilikataliwa.

Rodgers alitoa ofa ya paundi milioni 12 pamoja na kumtoa kiungo Jonjo Shelvey kwa mkopo, lakini dili hilo lilikataliwa na mwenyekiti wa Swansea, Hugh Jenkins.

Ingawa kocha huyo mpya wa Liverpool aliandika maafikiano na Swansea kwamba hatarudi klabuni hapo kwa nia ya kutaka kusajili mchezaji yeyote wa klabu yake hiyo ya zamani kwa kipindi cha miezi 12 ijayo, klabu hiyo Wales inaweza kukitosa kipengele hicho kama dili litakuwa na manufaa kwa klabu.
  

No comments:

Post a Comment