Monday, August 27, 2012

JEZI ZA MBUYU TWITE ZAGOMBEWA KAMA NJUGU WAKATI YANGA IKITUA LEO KUTOKA RWANDA BILA BEKI HUYO...!

Jezi za beki mpya wa Yanga, Mbuyu Twite zilikuwa zikigombewa kama njugu wakati wa mapokezi ya timu hiyo iliyotua leo jioni ikitokea Rwanda.

Hata hivyo, beki huyo 'kisiki' mwenye uraia wa Rwanda lakini aliye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo hakuambatana na wenzake leo na badala yake atatua nchini kesho, akimbatana na vibosile wa 'Wanajangwani' akiwamo Bin Kleb.

Mabingwa hao wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame), Yanga walitua jijini Dar es Salaam jana saa 9:00 alasiri.

Akizungumza baada ya kutua uwanjani hapo, kocha wa Yanga, Mbelgiji Tom Saintfiet, alisema kuwa Twite atatua kesho akiwa na wajumbe wa kamati ya utendaji ya klabu hiyo.
“Tunamshukuru Mungu kuwa tumerejea nchini salama. Wachezaji wamefanya kazi nzuri Kigali,tukiwa huko tulicheza mechi za kirafiki na bahati nzuri ni kwamba tulishinda zote,” alisema Saintfiet.
“Twite amebaki Kigali kumalizia masuala yake. Atakuja kesho (leo) na viongozi wa klabu ambao wamebaki naye huko,” aliongeza Saintfiet.


Akimuelezea beki huyo Mnyarwanda lakini mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Saintief alisema: “Ni mchezaji mzuri sana, alijiunga nasi kwenye mazoezi Alhamis. Nilimpanga katika mechi za kirafiki na alionesha kiwango cha juu. Nilikuwa nampa nafasi katika dakika 45 za kipindi cha pili kwa sababu hakuwa na mazoezi ya kutosha na hivyo tulimtumia kwa tahadhari ili asiumie.”

No comments:

Post a Comment