Wednesday, August 29, 2012

JAVI MARTINEZ HATIMAYE ATUA BAYERN, AVUNJA REKODI YA UHAMISHO UJERUMANI

Kiungo wa timu ya taifa ya Hispania, Javi Martinez akishangilia kombe la ubingwa wa michuano ya Mataifa ya Ulaya (Euro) 2012 baada ya kushinda mechi ya fainali 4-0 dhidi ya Italia kwenye Uwanja wa Olimpiki mjini Kiev, Ukraine Julai 1, 2012.

MUNICH, Ujerumani
BAYERN Munich wamekamilisha usajili wa kiungo wa Athletic Bilbao na timu ya taifa ya Hispania, Javi Martinez, klabu hiyo ya Bundesliga imetangaza leo, katika uhamisho ulioripotiwa kuweka rekodi ya Ujerumani ya euro milioni 40.

Martinez, 23, amevunja mkataba wake na Bilbao - ambao ulikuwa na kipengele cha kuuvunja cha euro milioni 40 - na ameruhusiwa kujiunga na Bayern na Shirikisho la Soka la Hispania (RFEF) na kampuni inayosimamia Ligi Kuu ya Hispania (LFP), Bayern imesema katika taarifa waliyoituma kwenye tovuti yao (www.fcbayern.telekom.de).

Amefuzu vipimo na yuko huru kuanza kuichezea klabu hiyo mara moja.

"Jambo hili limekwenda bila ya maswali hivyo sote tuna furaha kwamba Javi Martinez hatimaye yuko nasi," Mkurugenzi Mtendaji wa Bayern, Karl-Heinz Rummenigge amesema kuhusu hatma hiyo iliyofikiwa kufuatia mazungumzo yaliyodumu kwa majuma kadhaa.

Kabla ya Bayern kuthibitisha dili hilo, Bilbao ilisema katika taarifa yake kwamba Martinez amesafiri kwenda Ujerumani bila ya ruhusa yao jana kukamilisha uhamisho huo na kwamba wanamtaka ajieleze.

Akiwa amelelewa na Osasuna, Martinez alisajiliwa na Bilbao akiwa yosso mwenye umri wa miaka 17 mwaka 2006 na ameichezea timu ya taifa ya Hispania katika timu za rika zote. Alitamba msimu uliopita chini ya kocha Marcelo Bielsa, na kuisaidia timu yake kufikia fainali ya Kombe la Mfalme na fainali ya Ligi ya Europa. 


Bayern wamedhamiria kurejesha ubingwa msimu huu baada ya kumaliza wakiwa washindi wa pili katika Ligi Kuu ya Bundesliga na Kombe la Ujerumani msimu uliopita, wakibwagwa na Borussia Dortmund katika michuano yote.

No comments:

Post a Comment