Thursday, August 30, 2012

HAWA NGULUME AFARIKI DUNIA LEO... NI MKUU WA ZAMANI WILAYA ZA KINONDONI, BAGAMOYO, MBARALI... KUZIKWA KESHO GOBA, DAR ES SALAAM BAADA SWALA YA IJUMAA

Hawa Ngulume, enzi za uhai wake
Aliyewahi kuwa Mkuu wa Wilaya mbalimbali nchini, Bi. Hawa Ngulume, amefariki dunia jijini Dar es salaam leo saa 4:25 asubuhi, imefahamika.

Katibu Tarafa mstaafu wa Wilaya ya Kinondoni, Suleiman Mwenda, amesema mchana huu wakati akihojiwa na kituo cha televisheni ya taifa (TBC1), kuwa marehemu alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya kansa ya moyo na kwamba, amefariki dunia leo wakati akiwa kwenye Hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam.

Mwenda amesema kuwa mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Lugalo na mazishi yanatarajiwa kufanyika kesho nyumbani kwake Goba jijini Dar es Salaam baada ya kumalizika kwa swala ya Ijumaa, muda ambao wanatarajia vilevile kuwa ndugu zake kadhaa kutoka Singida watakuwa wameshafika kuhudhuria shughuli hiyo.

Mwenda amesema kuwa kabla ya kufariki dunia leo, marehemu aliwahi kutibiwa katika hospitali mbalimbali, ikiwamo ya Ocean Road ya jijini Dar es Salaam na pia aliwahi kwenda kutibiwa nchini India.
  
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana, amesema kuwa kifo cha Hawa Ngulume ni pigo kwani enzi za uhai wake alikuwa ni mchapa kazi hodari na tena mwenye ujasiri mkubwa; sifa zilizomuwezesha kuwahi kushika nafasi ya kuwa kiongozi wa wakuu wa wilaya.

Miongoni mwa wilaya alizowahi kuziongoza wakati akishikilia wadhifa wa ukuu wa wilaya kwa miaka 18 ni Kinondoni ya jijini Dar es Salaam, Bagamoyo mkoani Pwani na baadaye Mbarali mkoani Mbeya ambako ndiko alikostaafu kabla ya baadaye kuanza kusumbuliwa na maradhi.

No comments:

Post a Comment