Thursday, August 23, 2012

HUYU NDIYE REFA ATAKAYECHEZESHA 'EL CLASICO' YA BARCELONA NA REAL MADRID LEO KUANZIA SAA 5:30 USIKU KWA SAA ZA KIBONGO, ALIWAHI KUPIGWA CHUPA NA MCHEZAJI WA GRANADA MSIMU ULIOPITA AKIDAIWA KUIBEBA REAL MADRID KWA KUTOA KADI 2 NYEKUNDU NA PENATI ILIYOFUNGWA NA RONALDO...!

Refa Clos Gomez akiwa kazini
Mwache nimfundishe adabu... wachezaji wa Granada wakimzonga refa Clos Gomez wakati wa mechi yao dhidi ya Real Madrid, Mei mwaka huu.
Chukua hiyo... Clos Gomez akirushiwa chupa na mchezaji Benitez wa Granada ambayo ilimsababishia uvimbe kidevuni.
Refa atakayechezesha mechi ya kwanza ya 'el clasico' leo saa 5:30 usiku kati ya Barcelona na Real Madrid kuwania taji la Super Cup anaitwa Carlos Clos Gómez, aliyezaliwa Juni 30, 1972 katiika mji wa Zaragoza nchini Hispania.

Gómez alianza kutambuliwa rasmi kimataifa Januari 2009 baada ya kupata leseni daraja la pili ya Shirikisho la Soka la Ulaya (UEFA).

Kama ilivyo ada kibinadamu, mambo mabaya hupata nafasi ya kuvuma zaidi kuliko mazuri. Hali hiyo ndiyo humkuta Gómez mbele ya mashabiki wa soka kwani licha ya umahiri wake uwanjani, hukumbukwa zaidi kutokana na mechi ya Ligi ya Europa kati ya Motherwell na Steaua Bucureşti ambayo alivurunda na kupondwa sana na kocha wa wakati huo wa Motherwell, Jim Gannon.

Gómez anakumbukwa pia kwa tukio la mwaka 2008 wakati alipolazimika kuvunja mechi kati ya Real Betis na Athletic Bilbao baada ya mchezaji mmoja wa Bilbao kupigwa na chupa iliyorushwa na mashabiki kutokea jukwaani.

APIGWA CHUPA AKIDAIWA KUIBEBA REAL MADRID

Katika tukio mojawapo la kukumbukwa msimu uliopita (Mei 9, 2012) refa Gomez alijikuta katika wakati mgumu wakati akichezesha mechi ya La Liga, Ligi Kuu ya Hispania kati ya Granada waliokuwa wenyeji dhidi ya Real Madrid ambao walishinda mechi hiyo 'ngumu' kwa mabao 2-1.

Wachezaji wa Granada walikuwa wamemzunguka refa Gomez baada ya kutoa kadi mbili nyekundu za moja kwa moja wachezaji wao Guilherme Siqueira na Moises Hurtado wa Granada.

Kitendo hicho pia kilimkasirisha Daniel Benitez aliyechukua chupa ya plastiki iliyojaa maji ya ujazo wa nusu lita na kumtwanga nayo usoni. Wakati huo, Benitez (25), kiungo wa Mhispania, alikuwa ameshatolewa wakati wa mapumziko, lakini akajiingiza uwanjani wakati wa mabishano baina ya wachezaji wenzake wa Granada waliokuwa wakimzonga refa kulalamikia penati aliyowapa Real Madrid wakati zikiwa zimesalia dakika tisa kabla mechi kumalizika.

Cristiano Ronaldo alifunga penati hiyo ya goli la kusawazisha na baadaye Real wakaibuka washindi kutokana na goli la kujifunga la mabeki wa wenyeji katika dakika za majeruhi.

Baada ya mechi hiyo, Clos Gomez aliandika ripoti yake kama ifuatavyo:  "Mwishoni mwa mechi, wakati tukiwa bado uwanjani, mchezaji wa Granada Na. 24, Moises Hurtado aliniambia "wewe ni mwizi" na mimi nikamtoa nje. Nimemtoa nje pia kwa kadi nyekundu mchezaji wa Granada Na. 6, Guilherme Siqueira, kwa kuniambia "wewe ni mpuuzi". Baada ya kutoa kadi hizi mbili nyekundu, mchezaji wa Granada Na. 11, Daniel Benitez, alinirushia chupa iliyojaa maji ya ujazo wa 500 ml, akanisababishia uvimbe mdogo kidevuni, ambao hata hivyo haukuhitaji kupona kwa msaada wa dawa. Tulipokuwa tukielekea kwenye vyumba vya kuvalia, mchezaji wa Granada Na. 6, Guilherme Siqueira, aliniambia "mshenzi wewe!". Vilevile, mchezaji wa Granada Na. 22, Alex Geijo, aliniambia "umetuharibia malengo yetu yote ya msimu", wakati mchezaji wa Granada Na. 24, Moises Hurtado, wakati akiwa ameshavua jezi yake, alituzomea waamuzi wote wa mechi yao huku akisema "nyinyi ni wapuuzi".

Baadaye, mchezaji Benitez wa Granada alifungiwa miezi mitatu baada ya kukutwa na hatia ya kumtandika chupa Gomez.

No comments:

Post a Comment