Wednesday, August 1, 2012

EPIQ BONGO STAR SEARCH KUBEBA WASHINDI 17 DAR

Mmoja wa vijana waliojitokeza kushiriki katika shindano la kusaka vipaji vya kuimba la Epiq Bongo Star Search akionyesha uwezo wake wa kupiga gita lililotengenezwa kienyeji nje ya ukumbi kabla ya kukutana na majaji kwenye fukwe ya Coco jijini Dar es Salaam leo. 
Sehemu ya vijana waliojitokeza kushiriki katika shindano la kusaka vipaji vya kuimba la Epiq Bongo Star Search wakiwa nje ya ukumbi kabla ya kukutana na majaji kwenye fukwe ya Coco jijini Dar es Salaam leo.
Majaji wa shindano la kusaka vipaji vya kuimba la Epiq Bongo Star Search (kutoka kushoto) Salama Jabir, Ritha Paulsen na Master Jay, wakiwa "mzigoni" kwenye fukwe ya Coco jijini Dar es Salaam leo. 
Mshiriki wa BSS akijaribu bahati yake mbele ya majaji

ZAIDI ya vijana 5,000 wamejitokeza katika usaili wa shindano la kusaka vipaji vya kuimba la Epiq Bongo Star Search katika fukwe za Coco leo.

Usaili huo ambao utakuwa ni wa siku tatu umeonekana kuwa ni wa aina yake hasa kutokana na idadi kubwa ya vijana waliojitokeza jana ikiwa ndio siku ya kwanza.


Katika sehemu mbalimbali za uwanja huo ilionekana kujazwa na vijana hao ambao wengi wao walikuwa wakiimba huku wengine wakiwa wanafanya mazoezi ya kutumia aina mbalimbali za vifaa vya muziki.


Akizungumzia shindano hilo, jaji mkuu wa Epiq BSS, Ritha Paulsen alisema kuwa Dar es Salaam ambao ndio mkoa wa mwisho katika usaili huo hamasa imekuwa kubwa sana kwa washiriki huku wengi wao wakiwa na matumaini makubwa ya kuchaguliwa.


"Tumeona vijana wazuri sana, na kama kawaida ya Dar tunatarajia ushindani mkali kwa mkoa huu, na ndio maana tutachukua vijana kumi na saba kutoka hapa," alisema Ritha.


Afisa Biashara wa Zantel, Sajid Khan, amepongeza umati mkubwa wa watu uliojitokeza kwa upande wa Dar es Salaam akisema kwa vipaji vilivyopatikana mwaka huu watu watarajie burudani ya kutosha vipindi vikianza kuonyeshwa kwenye luninga.


"Tunatoa zawadi kubwa kwa mwaka huu, Sh. milioni 50 pamoja na mkataba wa kurekodi, hivyo vijana wana kila sababu ya kujitokeza kwa wingi kutimiza ndoto zao," alisema Khan.


Zoezi hili litaendelea siku ya kesho (Alhamisi) na kesho (Ijumaa) ambapo washiriki 17 watakaopatikana wataungana na wengine 33 kutoka mikoani kufikisha idadi ya washiriki hamsini watakaoingia kambini.

No comments:

Post a Comment