Wednesday, August 1, 2012

LISSU NA OLE SENDEKA BWANA...! NDANI YA BUNGE WANAWESHEANA MOTO KINOMA, NJE NI SHWAAARI!


'Acha kuleta zako hizoo...!' Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (kushoto) akizungumza nje ya Bunge na Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka (kulia) huku wabunge wengine wakiwatazama na kucheka jana
Wabunge nchini wanaenzi sana amani. Licha ya tofauti zao za mara kwa mara bungeni na ambazo wakati mwingine huongozwa zaidi na ushabiki wa vyama vyao kiasi cha kuzomeana na hata kushtakiana mbele ya Spika wa Bunge. bado waheshimiwa hao huonekana kuwa ni kama marafiki wawapo nje ya 'mjengo' wa Bunge.

Hali hiyo ilijidhihirisha jana wakati Mhe. Tundu Lissu, Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki (CHADEMA) alipoonekana nje ya 'mjengo' akichati bila hofu na Mbunge wa Jimbo la Simanjiro (CCM), Mhe. Christopher Ole Sendeka.

Ikumbukwe kuwa juzi, Mhe. Tundu Lissu alimlipua Ole Sendeka wakati akizungumza na waandishi wa habari, akimtaja kuwa naye ni miongoni mwa wabunge wanaotuhumiwa kwa kashfa ya kutanguliza maslahi yao binafsi na kutumiwa kuwatetea wafanyabiashara wa mafuta walionyimwa tenda ya kuiuzia TANESCO mafuta ya kuendeshea mitambo ya kufua umeme ya IPTL.

Kutokana na Lissu kumtaja Ole Sendeka juzi, Mbunge huyo wa Simanjiro alikuja juu na jana akaomba mwongozo wa Spika ili ajue kama ibara ya 100 inayotoa kinga kwa wabunge inaweza kumkwaza katika kutimiza dhamira yake ya kumburuza Tundu Lissu mahakamani kutokana na kile alichodai kuwa ni kumdhalilisha kwa kumzushia mbele ya waandishi wa habari kuwa anatumiwa kuwatetea wafanyabiashara wa mafuta.

Hata hivyo, wakati akitoa ufafanuzi juu ya mwongozo alioomba Ole Sendeka, Spika wa Bunge, Mhe. Anna Makinda, alisema kuwa anampeleka Tundu Lissu katika Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ili awe shahidi namba moja kuthibitisha tuhuma kwamba kuna wabunge wanaokula rushwa na kutumiwa na wafanyabiashara na pia wengine hutetea maslahi yao binafsi kwa kufanya biashara na TANESCO.

Spika alisema vilevile kuwa ibara ya 100 inamkinga Lissu dhidi ya kusudio la kuburuzwa mahakamani kwa vile alizungumza na waandishi wakati akiwa kwenye eneo la Bunge. Akawasihi wabunge kuwa na subira wakati kamati ya uongozi ikishughulikia tuhuma za kashfa ya rushwa dhidi ya baadhi ya wabunge, hasa wa kamati aliyoivunja ya Nishati na Madini.

Licha ya mgongano wao wa ndani ya Bunge, waheshimiwa Ole Sendeka na Tundu Lissu walionekana nje ya Bunge baadaye wakizungumza pamoja pasi na kuonyesha dalili zozote za uhasama baina yao. Yaani ilikuwa ni amani, hakuna shari.

Je, wabunge wa nchi nyingine kama Kenya wanaweza? Safi sana!




No comments:

Post a Comment