Thursday, August 23, 2012

DK. MWAKYEMBE NOMA...! AMPIGA CHINI MKURUGENZI MKUU WA BANDARI NA MAAFISA WENGINE WA VYEO VYA JUU... AAGIZA UCHUNGUZI MKALI UFANYIKE DHIDI YA VITENDO VYA WIZI... SASA ULE WIZI WA REDIO ZA MAGARI, "INDICATOR", "POWER WINDOW" KUBAKI HISTORIA....!

Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Banadari, Ephraim Mgawe
Kasi ya Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe katika kuhakikisha kuwa taasisi zilizo chini ya wizara anayoiongoza zinaondoa kero sugu zilizopo na kutekeleza majukumu waliyopewa kwa ukamilifu imeendelea tena leo baada ya kutua bandarini na kushusha rungu zito dhidi ya vigogo wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).

Kama alivyofanya hivi karibuni wakati alipotua Uwanja wa Ndege na kuwapiga chini viongozi wote wakuu, akiwemo Mkurugenzi Mkuu Paul Chizi, ndivyo alivyofanya leo baada ya kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Ephraim Mgawe na wasaidizi wake wawili ili kupisha uchunguzi wa kina kubaini ukweli juu ya tuhuma mbalimbali dhidi yao.

Mbali na Mgawe, wengine waliosimamishwa ni Meneja wa Mafuta ya Ndege Kurasini, Meneja wa JETTY na Meneja wa Oil Terminal ambao wote wameponzwa na tuhuma za kupotea kwa mafuta na pia kuidanganya serikali kuhusu taarifa za mafuta masafi na machafu.

Katika mtindo wake ule ule wa kata mpti, panda mti, Dk. Mwakyembe hakuchelewa kuteua bosi mwingine wa TPA baada ya kumteua Mhandisi Madeni Kipange kukaimu nafasi ya Mgawe.

Kama hiyo haitoshi, Mwakyembe ameunda tume maalum ya watu saba kuendesha uchunguzi mkali wa wiki mbili dhidi ya tuhuma kiabo zilizopo, zikiwemo za wizi na kwamba m,wishowe apelekewe taarifa yeye mwenyewe ofisini kwake.

Dk. Mwakyembe ambaye alisifika kwa kufanya kazi nzuri na ya kishujaa iliyomng'oa waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa na mawaziri Nazir Karamagi na Dk. Ibrahim Msabaha wakati alipoiongoza kamati ya Bunge iliyochunguza kashfa ya kampuni hewa ya kufua umeme ya Richmond, ameagiza vilevile kuwa kufikia tarehe 1 ya mwezi ujao, malipo yote bandarini yafanyike benki ili kukomesha vitendo vya rushwa na wizi unaofanywa ndani ya TPA.

Ameagiza pia kusimamishwa kwa Kampuni ya Singilimo yenye 'dili' la kubeba mafuta machafu na kutaka kazi hiyo ipewe kampuni nyingine itakayofanya kazi hiyo kwa ukamilifu.

Imeelezwa na baadhi ya wadau wanaotumia bandari ya Dar es Salaam kuwa hatua za Dk. Mwakyembe zinaweza kurudisha imani ya watumiaji ambayo sasa imepotea kwa baadhi yao kutokana na kukithiri kwa rushwa na wizi wa mizigo; hali ambayo imewalazimu baadhi ya wafanyabiashara kuikimbia bandari hiyo na kupitishia mizigo yao maeneo mengine kama Mombasa nchini Kenya.

Aidha, imeelezwa vilevile kuwa kwa kasi ya sasa ya Dk. Mwakyembe, haitachukua muda mrefu kukomesha pia wizi maarufu kwenye Bandari ya Dar es Salaam wa vifaa vya magari kama redio, "site mirror", "power window", taa kubwa na "indicator".

No comments:

Post a Comment