Monday, August 20, 2012

BOTI NYINGINE YAZAMA ZANIZIBAR IKITOKEA TANGA LEO, WATU 10 WAOKOLEWA, WENGINE WASAKWA... INAITWA MV. SARWAK

Ilivyokuwa boti ya Mv. Skagit baada ya kupinduka katika eneo la Chumbe na baadaye kuzama yote... hapa, baadhi ya abiria wakisubiri kuokolewa wakati ikiwa bado haijazama yote kwenda chini kwa umbali wa kina cha zaidi ya mita 60. Tukio hili lilijiri Julai 18.
Boti ndogo iitwayo Mv. Sarwak iliyokuwa ikisafiri kati ya Tanga na Zanzibar imezama leo na hadi sasa watu 10 wameokolewa na kukimbiziwa hopspitali visiwani humo huku wengine wawili wakiwa hawajulikani waliko.

Taarifa kutoka Zanzibar zimeeleza kuwa tayari msako dhidi ya watu hao wawili unaendelea na kwamba, majeruhi wako katika eneo la Vikokotoni visiwani humo.

Imeelezwa kuwa raia wawili kutoka Uholanzi na mmoja wa Ufaransa ni miongoni  mwa abiria 10 walionusurika baada ya kupatiwa 'life jacket' kabla ya kuzama kwa chombo hicho na baadaye kuokolewa.

Kwa mujibu wa manusura, boti hiyo ndogo ilizama baada ya pampu zake zinazotumika kuondoa maji kuharibika ghafla na hivyo maji kujaa wakati ikiendelea na safari kati ya eneo la Pangani, Tanga na Vikokotoni, Zanzibar.

Tukio hilo lililojiri leo limekumbushia ajali kubwa zaidi iliyotokea Julai 18 wakati meli ya Mv Skagit iliyokuwa ikitokea Dar es Salaam kuelekea Zanzibar ilipozama katika eneo la Chumbe na kusababisha vifo vya abiria wanaokadiriwa kuwa zaidi ya 200.

1 comment: