Friday, August 10, 2012

BOLT ASHINDA TENA MITA 200, ATAMBA: MIMI SASA NI GWIJI

Bolt akimaliza mbio za mita 200 na kutwaa medali ya dhahabu katika Michezo ya Olimpiki ya London

Bolt (katikati) akiwa na Wajamaica wenzake walioshika nafasi zote tatu za kwanza za mita 200, Yohan Blake (kushoto) aliyekuwa wa pili na Warren Weir (kulia) aliyeshika nafasi ya tatu.

USAIN Bolt amejitaja kwamba yeye sasa ni "mwanariadha bora zaidi" kupata kutokea duniani baada ya kutwaa medali yake ya pili ya dhahabu ya Olimpiki.

Baada ya kutetea medali yake ya mita 200, siku nne tangu alipotetea midali yake ya mita 100, alisema: "Mimi ni gwiji aliye hai."

Kabla ya hapo, Mjamaica huyo mwenye umri wa miaka 25, alisema alidhani kwamba ilikuwa inawezekana kuvunja rekodi yake mwenyewe ya dunia ya sekunde 19.19.

Baadaye, alikiri: "Nilikuwa na kasi lakini sikuwa fiti kiasi cha kutosha," kabla ya kuonya: "Siko tayari kustaafu. Naupenda mchezo huu."

Nchi ya Jamaica ilishika nafasi zote tatu za juu za mita 200, kwani pia Yohan Blake alishinda medali ya shaba na Warren Weir akitwaa fedha nyumba ya Bolt ambaye alitumia sekunde 19.32.

"Tulikuwa tukisukumana vyema na tuna furaha," alisema Bolt baada ya mbio hizo.

Ingawa hakuvunja rekodi yoyote ya Dunia wala ya Olimpiki katika mbio hizo, Bolt alijawa na furaha wakati akizungumza na wana habari, akisisitiza kwamba ameacha alama itakayodumu katika mchezo huo.

"Mimi sasa ni gwiji ninayeishi," Bolt aliongeza. "Sasa nitakaa, nitapumzika na kufikiria nini kitakachofuata.

"Sijajua hasa nini nataka kufanya baada ya hapa, kama ni kuendelea kukimbia mita 100 au 200 au kujaribu kitu tofauti. Nahitaji kutafuta lengo ambalo litanishawishi kufanya makubwa zaidi. Msimu uliobaki nitakuwa 'nakula bata' tu kwa sababu nimefanya kile kilichonileta hapa."

Bolt alikuwa mbele ya Mjamaica mwenzake Blake, 22, tangu mwanzo lakini alipunguza kasi wakati akikaribia kumaliza.

"Nilitokea kwenye kona, nilikuwa najisikia mwili kuvuta kidogo mgongoni, hivyo nilikuwa najaribu kudumisha kiwango changu," alisema. "Lakini nikaacha kukimbia kwa sababu nilijua haitakuwa rekodi ya dunia.

"Hakika nilitaka kuweka rekodi mpya katika mita 200, lakini nina furaha. Nilikuja hapa na nimejitoa kwa kila kitu na ninajivunia mwenyewe."

No comments:

Post a Comment