Thursday, July 19, 2012

YANGA YATINGA ROBO FAINALI BILA KUCHEZA

Mshambuliaji wa Yanga, Hamis Kiiza 'Diego' (kulia) akimchambua kipa wa Wau Salaam ya Sudan Kusini wakati wa mechi yao ya pili ya Kundi C la michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) 2012 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Jumanne Julai 17, 2012. Kiiza alifunga 'hat-trick' katika mechi hiyo ambayo Yanga ilishinda 7-1. Magoli mengine yalifungwa na Said Bahanuzi (mawili) na Stephano Mwasika. 
Kipa wa Mafunzo ya Zanzibar, Khalid Mahadhi Haji akidaka mpira wakati wa mechi yao ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati kwenyeUuwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam

Na Mwandishi Wetu
MABINGWA watetezi wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame), Yanga wametinga hatua ya robo fainali bila ya kucheza leo, kufuatia Wau Salaam ya Sudan Kusini kukubali kipigo cha 5-0 kutoka kwa Atletico ya Burundi kwenye Uwanja wa Taifa na kuaga mashindano hayo.

Kwa kuwa ni timu moja tu inayoaga kutoka katika kila kundi, Wau Salaam ambayo imeshiriki mashindano haya kwa mara ya kwanza imekuwa ya kwanza kutoka kutokana na kufungwa mechi zote tatu za Kundi C, ikiwa imepigwa jumla magoli 19-1. Ililala 7-0 katika mechi ya ufunguzi dhidi ya APR ya Rwanda kabla ya kukumbana na kipigo kingine cha 7-1 kutoka kwa Yanga Jumanne.

Yanga yenye pointi 3 inahitaji kushinda katika mechi yao ya kesho saa 10:00 dhidi ya APR iliyo na pointi 4, kama inataka kumaliza katika nafasi ya pili, nyuma ya Atletico ambayo imefikisha pointi saba baada ya ushindi wa leo.

Baada ya kuanza na kipigo cha 2-0 kutoka kwa Atletico, Yanga walifufuka katika mechi yao ya pili dhidi ya Wau Salaam kwa ushindi wa 7-1 Jumanne na wanahitaji kuthibitisha kesho kuwa hawakubahatisha kuifunga timu hiyo changa kutoka katika nchi ya Sudan iliyotawaliwa na vita kwa miaka mingi kabla ya kujitenga.

Vibonde wa Kundi A, Ports ya Djibout, ambao wamefungwa jumla ya magoli 10 huku wakiwa hawajafunga hata moja, wanatarajiwa kugawa pointi tena leo dhidi ya timu kali ya URA ya Uganda, ambayo ndiyo timu pekee yenye nafasi ya kumaliza kwa ushindi wa asilimia 100 mwaka huu. Ilianza kwa kuifunga Simba 2-0 kabla ya kuwachapa Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kwa mabao 3-1.

Simba wenye pointi 3 walizozipata katika ushindi wa 3-0 dhidi ya Ports jana, wako katika nafasi ya tatu ya msimamo kutokana na kuzidiwa wastani wa magoli na Vita yenye pointi tatu pia, ambayo ilishinda 7-0 dhidi ya Ports katika mechi ya ufunguzi wa Kundi A Jumapili.

Wekundu wa Msimbazi watawakabili Vita Jumamosi katika mechi inayotarajiwa kuwa ngumu.

Mafunzo ya Zanzibar imekaa kileleni mwa Kundi B kutokana na kufikisha pointi mbili baada ya sare yao ya pili dhidi ya Tusker ya Kenya wakati zilipotoka 0-0 mapema leo saa 8:00 mchana. Ilitoka pia sare ya 1-1 dhidi ya Azam. Timu itakayoaga kutoka kundi hilo itajulikana Jumamosi wakati Azam itakapocheza dhidi ya Tusker zote zikiwa na pointi moja-moja.  

No comments:

Post a Comment