Thursday, July 19, 2012

MAITI ZILIZOOPOLEWA ZAFIKIA 52, BOTI SASA YAZAMA CHINI NA WATU KWA UMBALI WA KINA CHA MITA 60

Wananchi wakiendelea na zoezi la utambuzi wa ndugu na jamaa zao leo kwenye viwanja vya Maisara, Zanzibar.
Baadhi ya maiti za watoto waliokufa katika ajali ya boti ya Skagit

Maiti zikishushwa garini leo baada ya kupatikana baharini katika tukio la jana la kuzama kwa boti ya Skagit.

Zoezi la kuandaa sanda kwa ajili ya miili ya watu ambao hawajatambuliwa kufuatia ajali ya boti ya Skagit likiendelea leo kwenye eneo la viwanja vya Maisara, Zanzibar. (Picha zote na Yusuf Simai wa MAELEZO, Zanzibar)

Habari kutoka katika eneo la uokoaji katika boti ya Skagit iliyozama jana kwenye eneo la Chumbe kisiwani Zanzibar zinaeleza kuwa hadi sasa, jumla ya miili ya watu walioopolewa imefikia 52.

Idadi hiyo ni kati ya watu 290 waliokuwamo ndani ya boti hiyo wakati ikisafiri kutoka jijini Dar es Salaam kuelekea Zanzibar, ambapo watu 146 kati yao wamesalimika baada ya kupatikana wakiwa hai.

Taarifa zilizotolewa bungeni leo asubuhi na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, zilieleza kwamba kutakuwa na siku tatu za maombolezo na katika kipindi hicho, bendera zote zitapepea nusu mlingoti.


BOTI SASA YAZAMA CHINI KABISA KINA CHA MITA 60


Abiria wa boti ya Skagit wakiwa juu ya chombo hicho baada ya kupinduka jana na kusubiri kuokolewa. Hapa ni kabla boti hiyo haijazama yote baharini na kwenda chini kwa umbali wa kina cha zaidi ya mita 60.
Katika hatua nyingine, imeelezwa kuwa zoezi la kufikia boti hiyo ili kuangalia uwezekano wa kuopoa baadhi ya maiti zilizonasia ndani ya chombo hico limeshindikana.

Taarifa hizo zimeeleza kuwa hivi sasa, boti hiyo imekwenda chini kabisa kwa kina cha umbali wa takriban mita 60 (zaidi ya urefu wa nusu uwanja wa soka), hivyo kushindikana kuifikia kwani uwezo uliopo kwa binadamu ni kwenda chini kwa umbali usiozidi mita 30.

Boti hiyo ya Skagit ambayo inamilikiwa na kampuni ya Seagul, ilizama jana baada ya kukumbwa na dhoruba kali, ikapinduka majira ya saa 7:00 mchana kabla ya kuzama yote baharini.

   

No comments:

Post a Comment