Monday, July 23, 2012

YANGA YATINGA NUSU FAINALI KAGAME, AKINA CHUJI WATISHA, WAFUNGA PENALTI ZOTE TANO


Stephano Mwasika (kulia) wa Yanga akiga mpira jirani na Ismail Khamis Amour wa Mafunzo ya zanzibar wakati wa mechi yao ya robo fainali ya Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo jioni.

Hamis Kiiza 'Diego' wa (pili kulia) wa Yanga akiwania mpira dhidi ya Mohamed Abdulrahman wa Mafunzo wakati wa mechi yao ya robo fainali ya Kombe la Kagame kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jioni hii.

Kipa wa Mafunzo, Halid Haji akiushuhudia mpira wa penalti ya Athumani Idd 'Chuji' ukienda wavunina kuipeleka Yanga kwenye nusu fainali ya Kombe la Kagame.

Asante Chujiiiiii.... mashabiki wa Yanga wakishangilia baada ya Athumani Idd 'Chuji' kufunga penalti ya mwisho iliyowapeleka Yanga kwenye nusu fainali jioni ya leo.


MABINGWA watetezi wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame), Yanga wametinga nusu fainali baada ya kushinda mechi yao ya robo fainali kwa penalti 5-3 dhidi ya Mafunzo ya Zanzibar kufuatia sare ya 1-1 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jioni ya leo.

Yanga sasa watacheza mechi ya nusu fainali dhidi ya APR Jumatano, baada ya Wanyarwanda hao kuwafunga URA ya Uganda 2-1 katika robo fainali ya kwanza iliyochezwa mapema saa 8:00 mchana leo. Hicho kilikuwa kipigo cha kwanza kwa URA ambayo ilikuwa timu pekee ilimaliza hatua ya makundi kwa ushindi wa asilimia 100.


Mafunzo ambao walitawala mechi leo, walitangulia kupata goli lililofungwa na Ali Othman Mmanga katika dakika ya 34 akihitimisha vyema kwa kichwa kona tatu mfululizo langoni mwa Yanga.


Straika mpya aliyejiunga na Yanga katika kipindi hiki cha usajili akitokea Mtibwa Sugar, Said Bahanuzi, alifunga bao lake la tano katika michuano hiyo mwaka huu kwa kichwa akiunganisha krosi ya beki mpya wa kulia, Juma Abdul. Bahanuzi sasa anaongoza ufungaji katika michuano hiyo akilingana na Taddy Etikiema wa APR.
Baada ya dakika 90, mechi hiyo moja kwa moja iliingia katika hatua ya kupigiana 'matuta' ambapo Yanga walitisha baada ya wachezaji wao wote watano kufunga penalti zao huku mmoja wa Mafunzo akikosa.


Wachezaji wa Yanga waliofunga penalti zao walikuwa Bahanuzi, Nadir Haroub 'Cannavaro', Hamis Kiiza, Haruna Niyonzima na Athumani Idd 'Chuji' wakati wachezaji wa Mafunzo waliofunga walikuwa Salum Shebe, Mohammed Abdulrahman na Jaku Juma Jaku. Said Shaban aligongesha nguzo.


Kiungo Rashid Gumbo, ambaye alipewa nafasi ya kuanza kutokana na kuumia kwa Nizar Khalfani, na mshambuliaji Jerry Tegete aliyeingia kuchukua nafasi yake katika dakika ya 51, walionekana kucheza chini ya kiwango, jambo lililoonyesha kumkera kocha mpya Mbelgiji Tom Saintfiet ambaye, bila ya kuwataja majina, alisema watasubiri sana kupata nafasi nyingine ya kucheza.
"Kuna wachezaji wamefadhaisha. Itabidi wafanye kazi kubwa sana ili kupata nafasi ya pili (ya kucheza)," alisema Saintfiet.
"Mafunzo ni timu nzuri, nilitaka tucheze kwa kasi kipindi cha kwanza lakini hatukuweza, wapinzani wetu wakatawala. Nilikuwa mkali sana wakati wa mapumziko, niliwataka wafunge haraka katika kipindi cha pili, wakafunga. Tulitaka tupate goli la pili lakini hatukuweza. Penalti ni 50-50, tulikuwa na bahati leo."


Kocha wa Mafunzo, Hemed Morocco, alisema wachezaji wake walicheza vizuri lakini walichoka kipindi cha pili kwa sababu wako katika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.


Yanga walimpoteza kipa wao, Yaw Berko baada ya kuumia katika dakika ya 72 na nafasi yake ikachukuliwa na kipa aliyejiunga akitokea Simba, Ali Mustapha 'Barthez'.


Michuano hiyo inaendelea kesho kwa mechi nyingine mbili za robo fainali ambapo mchana saa 8:00 Atletico ya Burundi itacheza dhidi ya AS Vita ya DRC, kabla ya Simba wakavaa Azam saa 10:00 jioni.


Vikosi katika mechi ya jioni vilikuwa; Yanga: Yaw Berko/ Ali Mustapha 'Barthez' (dk.72), Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub 'Cannavaro', Kelvin Yondani, Stephano Mwasika/ Idrissa Rashid (dk.64), Athuman Idd 'Chuji', Rashid Gumbo/Tegete (dk.51), Haruna Niyonzima, Hamis Kiiza na said Bahanuzi.


Mafunzo: Halid Haji, Suleiman Kassim 'Salembe', Ismail Amour/ Haji Hassan (dk.66), Said Shaaban, Salum Shebe, Ali Mmanga, Jaku Juma Jaku, Mohammed Abulrahman, Wahid Ibrahim/ Kheir Salum Kheir (dk.83) na Ally Hassan.  


----------

No comments:

Post a Comment