Monday, July 23, 2012

WAZIRI ATANGAZA KUJIUZULU JIONI HII KISA KUZAMA KWA BOTI YA MV SKAGIT


*DK. SHEIN AMKUBALIA, ATEUA WAZIRI MWINGINE KUTOKA CUF 
Waziri aliyejiuzulu, Hamad Masoud Hamad
Boti ya Mv Skagi ilivyokuwa ikionekana kabla ya kuzama yote baharini kwenye kina cha zaidi ya mita 60.

Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hamad Masoud Hamad ametangaza rasmi kujiuzulu wadhifa wake, imefahamika.

Akizungumza visiwani Zanzibar jioni ya leo,  Hamad amesema kuwa sababu ya kuchukua uamuzi huo ni dhamira yake ya kuwajibika kisiasa baada ya tukio la kuzama kwa boti ya Mv Skagit katika eneo la Chumbe visiwani Zanzibar.

Hamad alisema kuwa uamuzi huo aliuchukua siku moja tu baada ya kuzama kwa boti ya Skagit iliyozama Julai 19 na kumuandikia Rais wa Zanzibar, Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein juu ya dhamira yake hiyo.

Hamad akaongeza kuwa baada ya kumfikishia barua yake ya kuomba kujiuzulu, rais alimtaka asubiri na leo ameamua kutangaza baada ya kukubaliwa kwa ombi lake.

"Niliteuliwa na Rais kushika wadhifa huu mwaka 2010... baada ya miezi 20, sasa nimeamua kujiuzulu kisiasa badala ya kusubiri hadi tume iundwe," amesema Hamad.

Akielezea sababu za kuchukua uamuzi huo hivi sasa badala ya kuachia ngazi tangu ilipozama boti ya kwanza ya Mv Spice Islanders katika eneo la Nungwi na kuua mamia ya watu, Hamad alisema kuwa hakuchukua uamuzi huo wakati huo kwa sababu ndio kwanza alikuwa na miezi 10 tangu ateuliwe.

Wakati huohuo, imefahamika kuwa Rais Dk. Shein amekubali ombi la kujiuzulu kwa Hamad aliyetoka Chama cha Wananchi (CUF) na sasa kumteua Mhe. Rashid Seif Suleiman, Mbunge wa Ziwani (CUF) kutwaa nafasi yake.

Taarifa zaidi iliyotolewa jioni hii an Katibu wa Ikulu ya Zanzibar,  Abdulhamid Yahya Mzee imeeleza kuwa Serikali imeunda tume ya kuchunguza tukio la ajali ya kuzama kwa Mv. Skagit itakayoongozwa na mwenyekiti wake, Abdulhakeem Issa.

Boti ya Mv Skagit inayomilikiwa na kampuni ya Seagull Sea Transport Company Limited ilizama katika eneo la Chumbe wakati ikitokea jijini Dar es Salaam baada ya kupigwa dhoruba kali na kupinduka huku ndani yake ikiwa na watu zaidi ya 340.

Watu zaidi ya 100 wanahofiwa kufa na licha ya Serikali ya Zanzibar kusitisha zoezi la kusaka miili ya waliokufa, leo ilipatikana miili mingine ya watu watano.

No comments:

Post a Comment