Mhe. Hamad Masoud Hamad |
Chama cha Wananchi (CUF) kimeungana na
wananchi wengine mbalimbali kumpongeza Mhe. Hamad Masoud Hamad kwa hatua yake
ya kujiuzulu nafasi ya kuwa Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano wa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar ikiwa ni siku chache tu baada ya kuzama kwa boti ya Mv Skagit
na kuua mamia ya watu.
Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Sera
wa CUF, Salum Dimani, amesema kuwa chama chao, ambacho ndicho anachotoka Mhe.
Hamad, kimebaini kuwa waziri huyo wa zamani hakufanya kosa lolote, bali
amechukua hatua hiyo kwa nia ya kuwajibika kisiasa; hatua ambayo wametaka iigwe
na viongozi wengine wa juu pindi matukio ya namna hiyo yanapotokea.
Hamad alitangaza rasmi hatua yake ya
kujiuzulu jana na kusema kuwa aliandika barua hiyo tangu Julai 20 (siku moja
baada ya boti kuzama), lakini alitakiwa na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed
Shein kuwa afanye subira na jana ndipo akakubaliwa.
Jana, Dk. Shein alimteua Mwakilishi wa
Jimbo la Ziwani (CUF), Rashid Seif Suleiman kuwa mrithi wa nafasi ya Hamad
katika kuongoza wizara hiyo ya Miundombinu na Mawasiliano.
No comments:
Post a Comment