Maranda (kulia) na Farjala. |
Farjala (kushoto) na Maranda (mbele kushoto) wakisindikizwa katika korido za Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. |
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu,
jijini Dar es Salaam imewahukumu kwenda jela miaka 18 wafanyabiashara na ndugu
wawili, Rajabu Maranda ambaye alikuwa mweka hazina wa CCM mkoani Kigoma na
Farijala Hussein, baada ya wote kupatikana na hatia ya makosa sita kati ya saba
waliyokuwa wanakabiliwa nayo, yakiwemo ya kujipatia Sh bilioni 2.2 za Akaunti
ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Licha ya kutakiwa kwenda jela miaka
18, watatumikia miaka mitatu jela ambayo itakwenda sambamba pamoja na kifungo
cha awali cha miaka mitano kutokana na kifungo cha miaka mitatu kwa kila kosa,
ambayo ni kula njama, kughushi nyaraka, kuwasilisha hati bandia na kujipatia
Sh. 2,266,049,041.25.
Mahakimu waliosikiliza kesi hiyo walikuwa na hukumu
mbili tofauti. Ya kwanza iliandaliwa na Mwenyekiti wa jopo la mahakimu hao, Fatuma
Masengi ambaye ni Jaji wa Mahakama Kuu aliyepewa kibali na Jaji Mkuu Tanzania
kusikiliza kesi hiyo ambaye aliona washtakiwa hao hawana hatia.
Hukumu nyingine iliyotumika na
mahakama imeandaliwa na mahakimu wawili, Projestus Kahyoza na Katalina Revocat --
hii iliwatia wote wawili hatiani kwenye makosa sita kati ya saba yaliyokuwa
yakiwakabili.
Hakimu Kahyoza alisema wakati akisoma
hukumu hiyo kuwa, baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi saba wa upande wa
mashtaka, mahakama imeona kuwa pasi na shaka, washtakiwa hao wana hatia katika makosa
sita kati ya saba.
Alisema upande wa mashtaka umeweza
kuthitisha shtaka la kula njama kwa kuwa katika maelezo ya onyo ya mshtakiwa
Hussein ambayo yalipokelewa kama kielelezo na mahakama hiyo, yanaeleza kuwa
alipewa maelekezo na ndugu yake Maranda kuhusu kuandaa nyaraka za kughushi jina
la kampuni pamoja na mahali ambapo ofisi ya kampuni hiyo itakuwepo.
“Katika ushahidi ulitolewa na Jamhuri hapa
mahakamani, hakuna ubishi kama washtakiwa walighushi nyaraka za kusajili jina
la kampuni kutumia majina ya Paul Tobias na Fundi Kitunga, mahakama hii
inaamini shtaka hili kweli washtakiwa walighushi nyaraka hizo.”
Akielezea shitaka la kuwasilisha
nyaraka bandia, Hakimu Kahyoza alisema washtakiwa waliwasilisha nyaraka hizo
wakati huo (United Bank of Afrika (UBA) ambapo walifungua akaunti ya pamoja.
Alisema kwa kutumia majina ya uongo (Paul na Fundi), mahakama inaamini
washtakiwa walighushi hati ya kuhamisha deni wakionyesha ni wakala kutoka
Kampuni ya B.Graciel ya Ujerumani
kwenda Kampuni ya Money Planers & Consultant ya Tanzania.
Hakimu huyo alisema kuwa mahakama
inaamini washtakiwa waliwasilisha BoT hati za kughushi kwa ajili ya maombi ya
Sh. bilioni 2.2 ambazo walifanikiwa kuhamishiwa kupitia akaunti yao iliyokuwa
benki ya UBA. Aliongeza kuwa: "Mahakama inawaona washtakiwa hao hawana
hatia kwenye shtaka la sita la wizi ambalo hakuna shahidi wa upande wa Jamhuri
aliyethibitisha kama washtakiwa waliibia BoT.”
Aliongeza kwamba kutokana na maelezo
yote hayo hakuna ubishi kwamba washtakiwa walijipatia fedha kwa njia ya
udanganyifu baada ya kula njama, kughushi nyaraka na kuwasilisha hati bandia
BoT. Kwa upande wa Hakimu Masengi alisema katika hukumu yake ambayo itakuwa
kumbukumbu ya mahakama, ameona ushahidi uliotolewa na washtakiwa hauna nguvu ya
kuwatia hatiani na kwamba jukumu la kuthibitisha kesi ni la Jamhuri.
Alisema katika kesi hiyo, BoT
haijafika mahakamani hapo kueleza au kulalamika kama waliibiwa fedha hizo na
hata ile kampuni ya B.Graciel ya Ujerumani hawajalalamika kuibiwa fedha hizo na
washtakiwa. Hakimu Masengi alisema Wakala wa Majina ya Biashara (Brela)
hawajalalamika kupokea nyaraka zilizoghushiwa na washtakiwa mahakamani hapo na
kwamba ushahidi huo wa Jamhuri unaonyesha ni jinsi gani wameshindwa kuondoa
mashaka mbele ya mahakama hiyo.
Hakimu Revovat alisoma hukumu hiyo
kwamba washtakiwa wataanza kutumikia kiifungo hicho kuanzia jana sambamba na
kifungo cha awali. Katika kesi hiyo,washtakiwa wanadaiwa kuwa Machi 20 na
Desemba 25, mwaka 2005 washitakiwa walijipatia ingizo la Sh. 2,266,049,041.25
wakidai kwamba Kampuni ya B.Graciel ya Ujerumani imehamishiwa deni na Kampuni
ya Money Planers & Consultant ya Tanzania.
No comments:
Post a Comment