Tuesday, July 24, 2012

UBOVU VIWANJA VYA SOKA WACHEFUA WABUNGE


Juma Semsue wa Polisi Dodoma akibebwa na wenzake baada ya kufunga goli katika mechi mojawapo ya ligi kuu msimu uliopita kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.  

Sehemu ya Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro ambao hivi sasa unalalamikiwa kwa kuharibika vibaya kwenye eneo   
Hali mbaya ya viwanja vingi vya soka nchini vinavyomilikiwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) inaendelea kuwakera wabunge na baadhi yao wameitaka serikali kuvirejesha mikononi mwake kwani vinahatarisha usalama wa wachezaji na hata mashabiki wanaofika kushuhudia mechi mbalimbali za mchezo huo.

Wabunge wameyasema hayo leo asubuhi na mchana wakati wa kuchangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya ya mwaka wa fedha 2012/13 ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo huku wakiutaja uwanja wa Jamhuri Dodoma kuwa ni mfano wa viwanja hivyo vibovu kabisa na vinavyohatarisha usalama wa watumiaji wake.

Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Mhe.Grace Kiwelu, amesema sasa ni wakati mwafaka kwa CCM kufanya uamuzi wa busara wa kuvirudisha viwanja hivyo serikalini kama ilivyofanya kwa shule za sekondari zilizokuwa zikiendeshwa na Jumuiya ya Wazazi ya chama hicho.

Akitolea mfano Uwanja wa Jamhuri Dodoma, Mhe. Kihwelu alisema: “Umekuwa na hali mbaya kiasi ambacho hata wabunge wanaofanya mazoezi wapo hatarini kuumia viungo vyao.”

Alisema uwanja huo ambao upo katika makao makuu ya serikali na pia chama tawala (CCM), hauna hadhi ya kuitwa uwanja baada ya nyasi zake za kuchezea kutoweka na baadhi ya majukwaa kuvunjika.Mbunge wa Kinondoni, Idd Azzan (CCM), alisema viwanja vinavyomilikiwa na CCM kwa sasa havijiendeshi kibiashara na ndiyo maana vimechakaa kupita kiasi, hivyo serikali ichukue hatua ya kuvihudumia.

"Tunaomba serikali ivihudumie viwanja
hivi kwa sababu havijiendeshi kibishara, vipo kwa ajili ya kutoa huduma tu na ndiyo maana vinachakaa," alisema.

Viwanja vingine vya soka vilivyo aktika hali mbaya hivi sasa na baadhi kumilikiwa na CCM ni CCM Kirumba Mwanza, Ali Hassan Mwinyi Tabora, Jamhuri Morogoro, Majimaji Songea, Mkwakwani Tanga, Lake Tanganyika Kigoma,Umoja Mtwara, Samora Iringa, Sheikh Amri Abeid Arusha na Kambarage wa Shinyanga.

No comments:

Post a Comment