Tuesday, July 24, 2012

MAISHA PLUS YAREJEA KATIKA TV YAKO

Masoud Kipanya, mratibu wa shindano la Maisha Plus

Abdul kutoka Zanzibar, mshindi wa kwanza wa Maisha Plus 1

Steven Sandhu, alifika fainali ya Maisha Plus 1

MSIMU wa tatu wa mashindano ya maisha halisi ya katika televisheni ya Maisha Plus 2012 umeanza huku usaili wa kwanza kwa ajili ya kupata washiriki 21 watakaoingia katika kijiji cha mashindano ukipangwa kufanyika Agosti 3.

Masoud Kipanya, mratibu wa shindano hilo, ambaye pia ni mkurugenzi wa DMB Company Ltd inayoandaa Maisha Plus, alisema jijini Dar es Salaam jana mashindano hayo yatahusisha washiriki kutoka mikoa 13 na kwamba usaili utaanza Arusha Agosti 3, Moshi Agosti 4 na kisha Tanga utafanyika Agosti 5.

Mikoa mingine itakayofanyika usaili huo ni Dodoma, Morogoro, Iringa, Mbeya, Tabora, Shinyanga, Mwanza, Mtwara, Zanzibar na Dar es Salaam.

Moja ya mambo mapya katika Maisha Plus 2012 ni kwamba itakuwa na uhusiano na shindano la Mama Shujaa wa Chakula.

Mama Shujaa wa Chakula ni shindano linaloandaliwa na shirika la Oxfam. Shindano hili huwashindanisha wanawake wanaojihusisha na kilimo kidogo. Limewahi kufanyika mwaka jana na mshindi alikuwa ni Ester Jerome kutoka Dodoma, ambaye alijishindia zawadi ya trekta.

Unaweza kujiuliza "ni vipi Maisha Plus 2012 itashirikiana na Mama Shujaa wa chakula?", Masoud anajibu kwamba washiriki wa Mama Shujaa wa Chakula wataingia kijijini kabla ya vijana wa Maisha Plus, ambako watakaa kwa wiki mbili mpaka mshindi mshindi wao atakapopatikana. Baada ya hapo watatoka na ndipo shindano la Maisha Plus litakapoanza rasmi.

Alisema majaji wa Maisha Plus 2012 watakuwa ni Kaka Bonda, yeye mwenyewe Masoud Kipanya na Baby Madaha na kwamba shindano litaonyeshwa kila siku TBC1.

Kipanya aliongeza kuwa vigezo vya ushiriki ni umri baina ya miaka 21-26, awe Mtanzania bila ya kuzigatia rangi, elimu ya sekondari, mbunifu, ana ujuzi wa mawasiliano na mchapakazi.

Katika msimu wa kwanza wa Maisha Plus uliofanyika mwaka 2009, kijana Abdulhalim Hafidh wa Zanzibar aliibuka na mshindi na ilipofanyika kwa mara ya pili mwaka 2010, Alex wa Mbeya alishinda.

No comments:

Post a Comment