Monday, July 23, 2012

TP MAZEMBE YA MBWANA SAMATTA YASHIKWA


Mbwana Samatta wa TP Mazembe (kulia) akifanya vitu vyake katika moja ya mechi za klabu yake.
LUBUMBASHI, Kongo
MSHAMBULIAJI Emmanuel Clottey alifunga mara mbili na kuisaidia Berekum Chelsea ya Ghana kuishikilia TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa sare ya mabao 2-2 katika mechi yao ya Kundi B la Ligi ya Klabu Bingwa Afrika mjini Lubumbashi jana.


Clottey alifunga mara mbili katika kipindi cha pili na kuongeza idadi ya mabao aliyofunga katika michuano hiyo ya juu kwa ngazi ya klabu kufikia 11 wakati akiisaidia timu yake kusawazisha baada ya kuwa nyuma kwa mabao mawili hadi kufikia mwisho wa kipindi cha kwanza.


Matokeo hayo yameifanya klabu hiyo kuendelea kuwa wawakilishi wazuri wa Ghana, ikiwa ni mechi yao ya pili baada ya awali kushinda nyumbani kwao jijini Accra kwa mabao 3-2 dhidi ya vigogo wa Misri, klabu ya Zamalek.


Wakihitaji ushindi ili kujiongezea matumaini ya kufuzu kupitia kundi lao, TP Mazembe anayochezea Mtanzania Mbwana Samatta ilianza kwa kasi, ikiwabana wageni kwenye eneo la nusu ya uwanja wao. Walipata bao la utangulizi katika dakika ya 10 wakati nahodha wao Tresor Mputu Mabi alipofunga kwa shuti la karibu na lango na kuibua shangwe kwenye uwanja uliofurika mashabiki wa Frederic Kibassa Maliba.
Dakika chache baadaye, ‘besela’ liliwanyima bao Mazembe baada ya shuti kali la Mzambia Rainford Kalaba kuparaza na kutoka nje.


Katika dakika ya 31, wenyeji walipata goli la pili hatimaye kutokana na penati iliyopigwa na Mputu. Beki Edward Kpodo alidaiwa kumkwatua Mputu ndani ya eneo la hatari. Kipa Sowah wa Chelsea alipangua penati hiyo kabla Mputu kuwahi mpira huo na kufunga.


Berekum Chelsea walipewa penati katika dakika ya 70 baada ya kipa wa Mazembe, Muteba Kidiaba kumuangusha Clottey wakati alipobaki naye ndani ya eneo la 18. Clottey akafunga penati hiyo
Dakika sita kabla ya mechi kumalizika, Clottey (24), aliye katika kiwango chake cha juu cha ufungaji, alizima kelele za wenyeji wakati alipowatoka mabeki wawili wa Mazembe kabla ya kupiga shuti la kubetua lililompita Kidiaba na kujaa wavuni.

No comments:

Post a Comment