Severine George, mkazi wa jijini Dar es Salaam yuko njiapanda.
Ni baada ya jamaa zake wawili ambao ni raia wa Kenya kutokuwamo katika orodha
ya majina 340 iliyotolewa na Serikali leo na kuelezwa kuwa ndio waliokuwamo
ndani ya boti ya Skagit wakati ikizama juzi kwenye eneo la Chumbe wakati
ikitokea jijini Dar es Salaam kuelekea visiwani Zanzibar.
Akizungumza na Straika katika ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam leo ambako ndiko orodha ya watu hao ilikobandikwa na wananchi wenye
ndugu zao kupewa fursa ya kwenda kuiona, George anasema kuwa ameshangazwa kwa
kutowaona jamaa zake aliowataja kwa majina ya Mary Kiyoko na Benard Kalii.
Kwa sababu hiyo, George anasema kuwa amechanganyikiwa na
hajui awaambie nini ndugu walioko Kenya, ambao kila mara wamekuwa wakimpigia
simu kutaka kujua hatma ya watu hao.
Akieleza zaidi, George anasema kuwa juzi, yeye alishiriki
kuwasindikiza jamaa zake hao waliokuwa watatu na wote waliingia ndani ya boti
ya Skagit kuelekea Zanzibar.
Hata hivyo, anasema kuwa baada ya tukio la kuzama kwa boti
hiyo, aliyetambuliwa hadi sasa akiwa marehemu ni mwanamke mmoja ambaye alimtambua
kirahisi kwa vile anakumbuka namna alivyosuka nywele zake kwa kuzifunga rasta.
“Baada ya kutoonekana kwa hawa wawili (Kiyoko na Kalii), leo
nd’o nikadamkia hapa (katika ofisi za Mkuu wa Mkoa) ili niione orodha na kujua
hatua za kuchukua kulingana na maelekezo yaliyotolewa na serikali,” anasema
George.
“Hata hivyo, nimeshangazwa kuona kuwa katika orodha yote hii
ya majina yaliyoletwa na wenye boti (ya Skagit), sijaona jina la Mary wala
Benard… hapa nimechanganyikiwa. Simu
kutoka Kenya kuulizia hatma yao zimekuwa nyingi na sijui cha kuwajibu,” anasema George.
Akielezea kile anachodhani kuwa ndio chanzo cha kutokea
tatizo hilo la kutoonekana kwa baadhi ya majina, George anasema kuwa ni mfumo
mbovu uliokuwapo wa ukatishaji tiketi na uingiaji wa abiria ndani ya boti hiyo
kabla haijatoa nanga yake kwenye bandari ya Dar es Salaam.
Anaema kuwa kuwa hadi sasa, pale bandarini (Dar es Salaam) sijaona
ofisi rasmi za boti ya Skagit na kwamba, kilichotokea, wenye kutaka kusafiri
walikuwa wanapewa tiketi na watu waliokuwa katika eneo la bandari wakiwa na
makabrasha ya tiketi za boti hiyo.
“Kwa utoaji tiketi wa aina hii, wakati mwingine unaweza kuitwa
Severine lakini tiketi unayopewa ikawa imeandikwa Hassan… hapo kuingia kwenye boti huwa hakuna shida
kwa sababu kinachoangaliwa ni tiketi tu,” anasema George.
“Binafsi, kwa idadi ya watu niliowaona siku ile sidhani kama
walikuwa wa idadi hii inayotajwa (340), nadhani walizidi sana,” anasema.
George akavishauri vyombo vya dola kufuatilia suala hilo kwa
undani zaidi kwani kwa kutowaona jamaa zake wawili waliopanda boti hiyo,
anadhani kwamba huenda kuna watu wengine wengi waliokuwamo kwenye chombo hicho lakini
wakakosekana kwenye orodha hiyo ya watu 340.
Hadi kufikia jana saa 1:00 usiku wakati zoezi la uokoaji
likisitishwa, watu waliookolewa wakiwa hai walifikia 146 na miili iliyoopolewa
kufikia 52, ikiwemo miili 37 iliyoopolewa jana.
Serikali zote mbili, ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ya
Mapinduzi Zanzibar zilitangaza siku tatu za maombolezo kuanzia jana.
No comments:
Post a Comment