Wednesday, July 25, 2012

SUPER SPORT ITADHAMINI SOKA BONGO, ASEMA THOMAS MLAMBO


Mtangazaji wa Super Sport, Thomas Mlambo

MTANGAZAJI wa kituo cha televisheni cha Super Sport cha Afrika Kusini, Thomas Mlambo, amesema udhamini wa vituo vya televisheni una mchango mkubwa katika maendeleo ya soka na kwamba mambo yakikaa sawa, siku moja watakuja kudhamini Ligi Kuu ya Tanzania.

Mlambo amesema Super Sport ili kuonyesha Ligi Kuu ya Afrika Kusini, inalipa dola za Marekani milioni 3 (sawa na Sh. bilioni 7.2) kwa miaka mitatu, kiasi ambacho amesema kinasaidia sana katika klabu kujiendesha.

Amesema wanakwenda vizuri na mazungumzo na Rais wa TFF, Leodger Tenga, kwa lengo la Super Sport kuja kudhamini Ligi Kuu ya Tanzania Bara kiasi kwamba anatamani hata Tenga asiondoke madarakani, japo anafahamu kwamba hata akija kiongozi mwingine wataendelea walipofikia.

Alisema Ligi Kuu ya Tanzania Bara inavutia kudhamini kwa sababu ina timu kubwa kama Simba, Yanga na Azam, ambayo inakuja juu vizuri.

Aidha, kuhusu tatizo la Waafrika kupenda zaidi soka la Ulaya kuliko la kwao, Mlambo alivilaumu vyombo vya habari kwa kuchangia jambo hilo.

"Vyombo habari vya nchini kwetu vinatoa nafasi ndogo sana kwa habari za soka la Ulaya. Kwenye kurasa za michezo utakuta habari kubwa kuhusu nini Orlando Pirates wamefanya na habari kidogo mno ya nini timu ya Ulaya imefanya," alisema Mlambo wakati akihojiwa na watangazaji Gerald Hando na Paul James "PJ" wa kipindi cha Power Breakfast cha kituo cha redio cha Clouds FM leo asubuhi.  

"Hata ukija nyumbani kwangu. Katika kabati langu hutakuta jezi hata moja ya Chelsea au klabu ya Ulaya, ila utakuta fulana tano za Orlando Pirates. Ile ndio timu yangu ninayoshabikia."

Mlambo pia alizungumzia tatizo la wachezaji wa Afrika kudanganya umri, hasa baada ya wachezaji 15 wa timu ya taifa ya U-17 ya Nigeria kutokwa kikosini kutokana na kubainika kuzidi umri huo, na jinsi wanavyopambana nalo Afrika Kusini.

"Tatizo ni kwamba katika nchi nyingi za Afrika kijana anapata nyaraka yake ya kwanza akiwa na umri wa miaka 15 ndio maana anaweza kusema mimi ni mdogo kuliko umri wangu, nina miaka 13 au miaka 11.

"Matokeo yake utashangaa kuona mchezaji amechezea timu ya taifa ya vijana leo, lakini miaka 10 tu baadaye katika wakati ambao alipaswa kuwa na umri wa miaka 28, utakuta hata kutembea ni kwa shida (tayari ni mzee mno).

"Kwetu Afrika Kusini kila aliyezaliwa anasajiliwa. Na ili kucheza ni lazima ulete cheti cha kuzaliwa, cheti cha shule na vitu kama hivyo, inakuwa vigumu kudanganya umri."

Alipoulizwa anawatabiria nini Watanzania sita walioenda kushiriki Olimpiki inayofunguliwa rasmi kesho, Mlambo alisema, "natumai Afrika itafanya vizuri."

Mtangazaji huyo kipenzi cha mashabiki wa soka, pia alizungumzia nafasi ya makocha wa nyumbani kupewa nafasi katika kuendesha soka la Afrika.

"Naona klabu za hapa nyumbani zina makocha wa kigeni, (Tom) Saintfiet wa Yanga ni mzoefu. Soka la Afrika linawahitaji wageni hawa kwa ajili ya kuleta ujuzi zaidi, lakini pia tusiwadharau makocha wetu wa nyumbani tuwapeleke shule ili waje kuwa bora zaidi," alisema.

No comments:

Post a Comment