Wednesday, July 25, 2012

ARSENAL ITANUNUA WACHEZAJI WAPYA, ASEMA WENGER

*KUWAVAA MAN CITY KESHO

Arsene Wenger

LONDON, England
KOCHA wa Arsenal, Arsene Wenger amesema leo kuwa klabu hiyo ya Ligi Kuu ya England bado iko sokoni  na italeta nyota wapya kuimarisha kikosi chao.

Wenger, ambaye amewasajili Lukas Podolski na Olivier Giroud katika kipindi hiki cha usajili, hakuweka wazi ni nani anataka kumsajili lakini vyombo vya habari vya Uingereza vimemhusisha na mipango ya kumnasa winga wa Malaga na timu ya taifa ya Hispania, Santi Cazorla.

Mfaransa huyo alisema pia anatarajia kuwaona wachezaji wake majeruhi kama Jack Wilshere wakirejea wakiwa 'fiti' kikamilifu.

Wilshere, nguzo muhimu katika kiungo cha Arsenal, alikaa nje ya msimu mzima wa 2011-12 kutokana na majeraha ya 'enka' na anaendelea kupona.

"Niko tayari kuzungumza mengi, lakini sio mengi kuhusu usajili, kwa sababu jambo hili ni gumu sana na la siri sana," Wenger alisema katika tovuti ya Arsenal (www.arsenal.com).

"Tulimnunua Giroud na Podolski, na natuma 'tutamnunua' (Abou) Diaby na Wilshere pia, ambao hakucheza msimu mzima.

"Tutamuongeza Wilshere kikosini mapema iwezekanavyo. Lakini hatujafikia mwisho (wa usajili) -- tutaleta nyota wapya."

Wenger alisisitiza nia yake ya kumbakisha nahodha Robin van Persie klabuni.

"Hakuna cha kufafanua," Wenger alisema. "Machaguo yako wazi - tunataka kuwabakisha wachezaji wetu. Nitakuwa na furaha kwake kama atabaki kwenye Ligi Kuu ya England -- atabaki Arsenal."

Van Persie, ambaye ana mwaka mmoja umebaki katika mkataba wake Emirates, alitangaza mapema mwezi huu kwamba hataongeza mkataba.

Kama sehemu ya Arsenal ya kujiandaa na msimu mpya, kwa sasa wako katika mji mkuu wa China wa Beijing, ambako watacheza dhidi ya mabingwa wa Ligi Kuu ya England, Manchester City kwenye Uwanja wa Bird's Nest kesho.

No comments:

Post a Comment