Wednesday, July 25, 2012

ZITTO ATAKA MAKAMPUNI YA SIMU YAACHE KUWANYONYA KINA DIAMOND, ALI KIBA, NATURE, DIMPOZ, FEROUS, DULLY, MZEE YUSUF, JAY, MWASITI, DYNA

Diamond Platinumz
Ali Kiba (kulia) na Ommy Dimpoz
Mzee Yusuf
Mwasiti
Sir Juma Nature
Dully Sykes
Mhe. Zitto Kabwe

Mhe. January Makamba
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Mhe. Zitto Kabwe ameitaka Serikali iyabane makampuni yote yanayotoa huduma za simu nchini ili yaache tabia wanayoendelea nayo sasa ya kuwanyonya wasanii kwa kuwalipa fedha kiduchu pindi wanapouza milio ya nyimbo zao kupitia simu za mkononi.

Zitto aliyasema hayo leo mchana na kisha akacharukia tena suala hilo jioni hii wakati akichangia hoja ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia.

Akielezea kile alichodai kuwa ni dhulma, Mhe. Zitto alisema kuwa hivi sasa, makampuni ya simu yamekuwa yakifaidika zaidi na biashara hiyo ya kuuza nyimbo za wasanii kupitia 'ring tone' za simu huku wenyewe (wasanii) wakiambulia fedha kidogo sana.

Alifafanua kwamba kwa mgawanyo wa sasa, makampuni ya simu hujitwalia asilimia 80 ya mapato yatokanayo na mauzo ya kila wimbo huku wasanii huishia kuambulia asilimia saba tu na kuna kiasi kingine huangukia kwa "watu wa kati"; jambo alilodai kwamba haliwatendei haki vijana wenye nyimbo hizo kwani huhangaika sana ili kukamilisha nyimbo zaop

"Mgawanyo huu haukubaliki. Tuamue kwamba kaunzia sasa, ni afadhali wasanii wenyewe wapate walau asilimia hamsini... kama yapo makampuni yatakayowaongezea itakuwa vizuri, lakini isiwe chini ya asilimia hamsini," alisema Zitto.

Akijibu hoja ya Zitto ambaye aliibua tena suala hilo wakati Bunge lilipokaa kama kamati, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Januari Makamba, alisema kuwa hoja ya Zitto ni ya msingi na serikali itaifanyia kazi.

Makamba alieleza zaidi kuwa, kwavile suala hilo linahusisha pia wizara nyingine kama ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, watalijadili kabla ya kumalizika kwa vikao vya sasa vya bunge kwani anajua kuwa wakichelewa, wasanii wataendelea kudhulumiwa.

Miongoni mwa wasanii maarufu ambao nyimbo zao zimekuwa zikitumiwa na makampuni ya simu kwa kuziuza kupitia milio (ring tone) ni pamoja na Diamond, Ali Kiba, Mzee Yusuf, Prof. Jay, Sir Nature, Ommy Dimpoz, Mwasiti, Dyna, Mzee Yusuf, Ferous, Dully Sykes, Chegge na Mhe. Temba    

No comments:

Post a Comment