Monday, July 30, 2012

SOMA TAMKO LA SERIKALI KUHUSU MGOMO WA WALIMU ULIOANZA LEO


WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI

TAMKO LA WAZIRI WA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI KUHUSU MGOGORO ULIOWASILISHWA NA CHAMA CHA WALIMU TANZANIA (CWT)
Serikali kupitia Ofisi ya Katibu Mkuu kiongozi ilipokea notisi ya saa 48 ya kusuduio la wanachama wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kugoma Kuanzia Jumatatu tarehe 30.07.2012.  Notisi hii ilipokelewa Ijumaa tarehe 27/07 saa 9 alasiri.    Mgogoro huo unaelezwa na CWT kuwa unatokana na Serikali kushindwa kutimiza madai ya Walimu ambayo wameyataja kuwa  ni:
                             i.        Nyongeza ya mshahara ya asilimia 100 kwa walimu wote nchini;
                            ii.        Kulipwa posho ya kufundisha kwa walimu wa sayansi asilimia 55 na walimu wa sanaa asilimia 50; na
                          iii.        Kulipwa posho ya mazingira magumu asilimia 30 kwa walimu wanaofanya kazi katika mazingira magumu.2.0   HATUA ZILIZOCHUKULIWA
Mgogoro huu ulisajiliwa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi  (Commission for Mediation and Arbitration – CMA).  Tarehe 26 Juni, 2012, kikao cha kwanza cha usuluhishi kati ya CWT na Serikali kilifanyika chini ya Msuluhishi wa Tume.  Katika Kikao hicho ilikubalika kuwa CWT iandae na kuwasilisha hati ya ufafanuzi wa madai yake na Serikali itoe majibu kabla au ifikapo tarehe 9 Julai, 2012.

Kikao cha pili cha usuluhishi kilifanyika tarehe 10 Julai, 2012 kama ilivyopangwa na pande zote mbili zilitimiza matakwa ya Msuluhishi. CMA iliomba serikali iwasilishe mapendekezo (offer) ya kiwango ambacho inaweza kukiongeza kwa kuzingatia madai ya CWT. CMA ilipendekeza majadiliano yaendelee tarehe 20/07/2012.

Tarehe 20/07/2012 serikali iliwasilisha mapendekezo (offer) kuwa imeongeza mshahara wa walimu kwa wastani wa asilimia 14 tofauti na watumishi wengine ambao wamepata nyongeza ya wastani wa asilimia 13 kiwango ambacho kilifikiwa katika mjadala wa nyongeza za mishahara ya watumishi wa umma (Public Service Joint Staff Council) ambao CWT ni wajumbe na walihudhuria. Nyongeza hiyo ya walimu imetokana na utaratibu wa serikali wa kuboresha mishahara kwa watumishi wa umma. Vilevile, Serikali ilitoa taarifa kuwa imeunda  Bodi ya Mishahara  na Maslahi kwa ajili ya kumshauri  Mhe. Rais juu ya misingi ya mishahara katika utumishi wa umma. Bodi imeanza kazi tarehe 01 Julai 2012 na inahitaji muda wa kufanya kazi na kuja na mapendekezo ambayo yatatumika kuboresha mishahara na maslahi ya watumishi wa umma wakiwemo walimu. CWT walikataa mapendekezo (offer) hayo na Msuluhishi alitoa uamuzi wa kushindwa kusuluhisha mgogoro huo na kuziomba pande zote mbili kufika Tume tarehe 25/07/2012 kwa ajili ya kuchukua cheti cha uamuzi kushindwa kusuluhisha (certificate of Deadlock).
Baada ya Serikali kutafakari athari za mgomo na kwa kuzingatia kuwa Chombo ambacho kilipaswa kupokea na kujadili madai ya CWT ambacho ni “Teachers Service Joint Staff Council”  hakikuwepo.  Tarehe 26 Julai 2012 Serikali iliwasilisha Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi  maombi ya kuzuia mgomo pamoja na kuwataka CWT kurudi katika meza ya mazungumzo ili kuruhusu madai ya CWT kushughulikiwa na chombo  kilichopaswa kufanya hivyo kisheria. Maombi hayo yalisikilizwa siku ya Ijumaa tarehe 27Julai 2012 na pande zote mbili ziliagizwa kukamilisha maelezo na kuyawasilisha Mahakamani. Serikali ilipangiwa  kuwasilisha maelezo yake siku ya Jumatatu tarehe 30 Julai 2012 saa nne asubuhi na CWT ilipangiwa kuwasilisha maelezo yake siku ya Jumanne tarehe 31 Julai 2012 saa sita mchana na shauri hilo litasikilizwa saa saba mchana.

3.0 MAMBO AMBAYO YAMEKUWA YAKIJITOKEZA
Katika kipindi ambapo CWT iliwasilisha kusudio la mgogoro na hatimaye kusajili Tume ya Usuluhishi na Upatanishi (CMA), kumekuwa na ushawishi kutoka katika vikundi mbalimbali kuhamasisha mgomo wa walimu wote nchi nzima endapo Serikali itashindwa kutimiza matakwa ya CWT.  Ushawishi huo umekuwa ukifanyika kwa njia mbalimbali zikiwemo za ujumbe mfupi wa simu  na  kupitia vyombo  vya habari. 

Aidha, kumekuwa na ujumbe unaopotosha ukweli unaosambazwa kwenye simu za viganjani na magazeti unaoonesha kuwa kada za ualimu wanapata viwango vya chini vya mshahara ikilinganishwa na kada za Afya, Utafiti, Kilimo / Mifugo na Sheria japo wana  sifa za kitaaluma zinazofanana. Ujumbe huo una lengo la kupotosha umma na hususan walimu ili kushawishi kuungwa mkono na walimu ambao wengi hawana taarifa sahihi kuhusu suala hilo.
4.0   TARATIBU ZA MIGOMO KISHERIA
Sheria ya Majadiliano ya Pamoja Katika Utumishi wa Umma Sura 105 Kifungu cha 26 (1) na (2) kimefafanua utaratibu utakaofuatwa wakati watumishi wa Umma wanapotaka kufanya migomo / kumfungia nje mwajiri.  Masharti hayo ni;
            (i).    Kuwepo na mgogoro au malalamiko,
           (ii).    Mgogoro huo uwe umeshindwa kupata suluhu,
          (iii).    Kura ya kukubali kufanya mgomo iwe imepigwa na watumishi wengi wa sekta husika chini ya usimamizi wa Afisa kazi, na
         (iv).    Notisi ya siku sitini ya kusudio la kufanya mgomo iwe imewasilishwa Serikalini baada ya siku ya kura ya nia ya kufanya mgomo.kufanyika.
Mtumishi yeyote atakayekiuka masharti tajwa hapo juu anaweza kuchukuliwa hatua za kinidhamu.
Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na.6 ya mwaka 2004 chini ya Kifungu cha 80 kinatoa haki na masharti ya kufuata pale mtumishi anapotaka kujiunga na mgomo.  Masharti hayo ni;
        (i).        Kuwepo na mgogoro wa kimaslahi;
           (ii).    Mgogoro uwe umewasilishwa tume ya usuluhishi;
          (iii).     Mgogoro huo uwe umeshindwa kupata suluhu ndani ya siku thelathini kwa mujibu wa kifungu cha 86 (4) kikisomwa pamoja na kifungu cha 87 (1&2);
         (iv).    Mgomo uwe umeitishwa na chama cha wafanyakazi na kuungwa mkono na wanachama wengi kwa mujibu wa katiba ya chama; na
          (v).    Wafanyakazi pamoja na chama watoe notisi ya saa 48  ya kusudio la kufanya mgomo kwa mwajiri.
Sheria zote hizo  mbili zimetoa taratibu zinazotofautiana endapo mtumishi / chama kinapotaka kujihusisha katika mgomo.  Kutofautiana kwa taratibu hizo, kumeifanya CWT kuchagua utaratibu chini ya  Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na.6 ya mwaka 2004 ambao  mchakato wake ni mfupi zaidi.  Aidha, kwa mujibu wa kifungu cha 83(4) g cha Sheria  hiyo,  mwajiri hatalazimika kulipa mshahara kwa mtumishi aliyeshiriki katika mgomo kwa kipindi ambacho mtumishi atakuwa kwenye mgomo.
5.0      ATHARI ZA MGOMO
Migomo huleta athari mbalimbali katika jamii husika ikiwemo:
·        Wanafunzi kukosa haki yao ya msingi ya  kufundishwa na kujifunza  na kusababisha matokeo mabaya ya mitihani; na
·        Uvunjifu wa amani katika sehemu za kazi.

6.0      HITIMISHO
Kwa vile shauri hili bado lipo Mahakamani, mgomo wa Walimu kwa sasa ni batili. Tumepokea taarifa za watu kunyanyaswa, kupigwa na kuharibiwa mali zao na mali za Serikali kunakofanywa na baadhi ya walimu ambao wanataka kuendelea kususia kufundisha.
Jambo hili si sawa na si busara kwa mtu mwenye taaluma ya ualimu kujihusisha na vitendo vinavyokwenda kinyume na sheria na taratibu kwa maslahi yake binafsi. Tunapenda kuwahakikishia wananchi wote na walimu ambao hawajajihusisha na vitendo hivi kuwa serikali na vyombo vya ulinzi na usalama vitawalinda na kuwahakikishia usalama wao.
Lakini pia tunapenda kuwatahadharisha wote wanaojihusisha na vitendo viovu kama kuwatisha wenzao, kuwapiga, kuwaharibia mali au kwa njia yoyote kuwanyanyasa kwa sababu ya kuwa hawajawaunga mkono kugomea kufundisha kuwa, serikali itachukua hatua kali dhidi yao. Serikali inatoa onyo kwa baadhi ya walimu ambao wanashawishi na kuwatumia wanafunzi katika mgogoro huu, hii si sawa na sihaki kabisa. Wanafunzi wasihusishwe wala kutumiwa kwani mgogoro huu ni baina ya Serikali na walimu.
Mwisho tunapenda kuwasihi wazazi na walezi kuwa wasikubali, wawazuie na wawakataze watoto wao kutumiwa au kuhusishwa kwenye mgogoro huu ambao utawahatarishia usalama na maisha ya watoto wao.
MWISHO

No comments:

Post a Comment