Monday, July 30, 2012

HISPANIA YAAGA KWA AIBU, NEYMAR "HAFAI"


Mshambuliaji wa Uruguay, Luis Suarez (katikati) akishindwa kufunga dhidi ya kipa Ousmane Mane wa Senegal (kulia) baada ya Saliou Ciss (kushoto) kuzuia mpira huo wakati wa mechi yao ya Kundi A la Michezo ya Olimpiki ya London 2012 kwenye Uwanja wa Wembley mjini London jana Julai 29, 2012. Picha: REUTERS
Kadi nyekundu.... Mshambuliaji wa Uruguay, Luis Suarez akichezewa faulo na Abdoulaye Ba wa Senegal (kulia) wakati wa mechi yao ya Kundi A la Michezo ya Olimpiki ya London 2012 kwenye Uwanja wa Wembley mjini London jana Julai 29, 2012. Ba alitolewa kwa kadi nyekundu kwa faulo hiyo, lakini Uruguay bado "walikalishwa" 2-0. Picha: REUTERS
Mshambuliaji wa Mexico, Giovani dos Santos akishangilia baada ya kufunga goli dhidi ya Gabon wakati wa mechi yao ya Kundi B la Michezo ya Olimpiki ya London 2012 kwenye Uwanja wa City of Coventry jana Julai 29, 2012. Picha: REUTERS

LONDON, Uingereza
NDOTO ya Hispania kutwaa ubingwa wa Olimpiki na kujumuisha katika mataji yao ya Dunia na Ulaya, ilizimika kwa aibu jana Jumapili baada ya kipigo cha kustisha cha 1-0 kutoka kwa Honduras na kuwaacha wakiwa hawana nafasi ya kutinga hatua ya mtoano.

Timu inayopewa nafasi ya kutwaa ubingwa wa Olimpiki ya Brazil, ikibebwa na mshambuliaji mwenye kipaji Neymar, ilitangulia robo fainali baada ya kuzinduka kutoka nyuma na kuifunga Belarus 3-1 kwenye Uwanja wa Old Trafford huku Neymar akifunga goli moja na kupika mawili mengine.

Walifuatwa katika hatua ya 8-Bora na Japan, ambao walinogesha ushindi wa 1-0 dhidi ya Hispania Alhamisi kwa ushindi mwingine dhidi ya Morocco.

Hispania iligongesha nguzo za lango la Honduras mara tatu baada ya kuruhusu bao la mapema kwenye Uwanja wa Newcastle.

Walilalamikia kunyimwa penalti mbili za wazi na baada ya firimbi ya mwisho walimzunguka refa wakionyesha kukerwa na maamuzi yake.

Kikosi hicho cha Hispania cha Under-23 mjini London kilijumuisha wachezaji watatu wa timu ya wakubwa ambayo ilitetea taji lao la Mataifa ya Ulaya Julai 1.

Kocha wa Hispania, Luis Milla, alipoulizwa kama mafanikio ya timu yao ya wakubwa iliongeza presha kwenye kikosi chake, alisema: "Ndio inawezekana kwamba presha imechangia matatizo kwetu, lakini hii ni timu iliyojaa wachezaji ambao wanashindana katika ngazi ya juu.

"Kama makocha tutaangalia kwanini tumetolewa. Tuko nje ya Michezo ya Olimpiki - lakini tlijiandaa vyema sana kwa michuano hii. "

"Kama unavyoona kila mtu amefadhaika sana. Tulifanya kazi nzuri, tulicheza vyema na kuonyesha soka zuri na bado tunaendelea kuiamini staili yetu ya uchezaji."

Honduras ilipoteza mechi zote tatu za hatua ya makundi katika michuano hiyo ilipofanyika mjini Beijing miaka minne iliyopita lakini walikaza msuli baada ya krosi ya Roger Espinoza kutokea kushoto kutua kichwani mwa Jerry Bengtson ambaye aliruka juu kiufundi akimpiku Jordi Alba na kuusukumiza wavuni mpira uliompita kipa wa Manchester United, David De Gea.

"Ilikuwa ni kipindi cha pili chenye presha kubwa. Walitengeneza nafasi nyingi sana za kufunga na tulifanya vyema wakati walipotishia kutufunga," alisema Bengtson. "Ilikuwa ni kazi ngumu sana lakini tumefanya vyema na kuwafunga."

Wenyeji Great Britain walishinda mechi yao ya kwanza ya Olimpiki tangu waliposhiriki katika Michezo ya Rome mwaka 1960, wakicheza vyema na kuizima timu iliyojaa hamasa ya Falme za Kiarabu kwa mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Wembley.

Goli lao la kwanza lilifungwa na nahodha Ryan Giggs, ambaye akiwa na umri wa miaka 38 na siku 243 ameweka rekodi ya mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi kushiriki fainali za Olimpiki katika soka na mfungaji bao mkongwe zaidi baada ya kupachika goli kwa kichwa katika dakika ya 16.

Great Britain walikamilisha ushindi kwa magoli ya dakika za lala salama kutoka kwa mchezaji aliyeingia akitokea benchi Scott Sinclair na Daniel Sturridge na kuongoza Kundi A kwa wastani wa mabao dhidi ya Senegal ambao waliwashangaza Uruguay kwa kuwachapa 2-0 katika mechi ya kwanza kwenye Uwanja wa Wembley.

Ushindi huo ulikuwa wa kukumbukwa zaidi kwani Senegal walipunguzwa na kubaki kumi 10 wakati Abdoulaye Ba alipotolewa kwa kadi nyekundu kwa kumuangusha nahodha  wa Uruguay, Luis Suarez katika dakika ya 30.

Magoli mawili kutoka kwa Moussa Konate kabla ya mapumziko yalitosha kuishushia Uruguay, iliyorejea kwenye Olimpiki kwa mara ya kwanza tangu ilipotwaa ubingwa mara mbili wa michuano hiyo mwaka 1928, kipigo cha kwanza cha kabisa cha kihistoria Olimpiki. Ilikuwa haijawahi kufungwa katika Olimpiki.

KIWANGO CHA HAMASA
Brazil ilikuwa timu ya kwanza kutinga hatua ya 8-Bora na kiujumla walistahili ushindi dhidi ya Belarus, kupitia goli la kichwa kutoka kwa Alexandre Pato kufuatia krosi ya Neymar, goli tamu la 'fri-kiki' la umbali wa mita 30 kutoka kwa Neymar na bao la tatu lililofungwa kiufundi na Oscar baada ya kutengewa kwa pasi ya kisigino na Neymar.

Mzaliwa wa Brazil Renan Bardini alifunga kwa kichwa goli la kuongoza la Belarus katika dakika ya nane lakini licha ya kufungwa watasonga mbele kama watawafunga Misri keshokutwa Jumatano.

Misri walipoteza nafasi kibao katika sare ya 1-1 dhidi ya New Zealand kwenye Uwanja wa Old Trafford ambayo iliwafanya nafasi zao za kusonga mbele kuwa finyu.

Katika mechi nyingine, Mexico iliifunga Gabon 2-0 mjini Coventry kupitia kwa magoli mawili ya mshambuliaji wa Tottenham, Giovani Dos Santos.

Mexico wana pointi nne katika Kundi B na wanaonekana kujiandaa kutinga hatua ya robo fainali, pengine na Korea Kusini ambao waliwafunga Uswisi 2-1 na ambao pia wana pointi nne.

No comments:

Post a Comment